Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tumalize mwaka kwa nidhamu ya fedha

Fedhapic Tumalize mwaka kwa nidhamu ya fedha

Wed, 29 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zimebaki siku mbili kumalizika mwaka 2021, ukiwa ni msimu wa sikukuu mbili Krismasi iliyosherehekewa Desemba 25 na Mwaka Mpya itakayosherehekewa Januari Mosi, 2022 na kufungua mlango wa kutimiza malengo ya mwaka mwingine mpya.

Kwa kawaida msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka huambatana na harakati nyingi kuliko wakati mwingine wa mwaka sambamba na matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kusherehekea sikukuu hizo, lakini mbali na hayo msimu huu pia huenda sambamba na maandalizi ya wanafunzi kurejea shuleni.

Ni katika wakati huu pia ambao wazazi wanapaswa kujiandaa kwa ajili ya kulipa ada za watoto wao ili waweze kurejea shule

bila bughudha na kuendelea na masomo. Ni wakati huu pia ambao tunashuhudia vibonzo vikisambaa mitandaoni kuwakumbusha watu kuhusu kulipa ada za watoto ili kuepukana na aibu za watoto kubaki nyumbani au kukumbwa na fedheha za kwenda kuzungumza na wahasibu na wamiliki wa shule wawavumilie kwa muda ili wakamilishe ada wanazotakiwa kulipa.

Unaweza kufikiri kwamba vibonzo hivyo ni sehemu ya utani wa maisha ili kuburudisha baraza, lakini kuna ukweli ndani yake kwa maana wapo watu ambao wanatumia fedha bila kuweka sawa bajeti ya maandalizi ya shule ya watoto wao na kujikuta wakipata shida shule zinapokaribia kufunguliwa.

Huu ndio wakati baadhi ya wazazi ambao hawajajiandaa vema kurejesha

watoto wao shuleni kuanza kuhaha na kuchanganyikiwa kutokana na kushindwa kujipanga katika vipato vyao na kujikuta wakitumia fedha nyingi kwa ajili ya sikukuu zaidi ya bajeti inayowakabili na kujikuta wakishindwa kulipa ada za watoto.

Wengine hufika mbali zaidi kiasi cha kushindwa hata kutoa huduma muhimu za familia zao na kujiingiza katika madeni ambayo hawakuyatarajia ili tu watoto wao waweze kwenda shule hali inayopelekea mtu ajikute akishindwa kujipanga vema kiuchumi kwa miezi kadhaa ya mwanzo wa mwaka.

Wakati umefika wazazi wajue kwamba kujipanga na kutumia fedha kwa kadiri ya bajeti na kipato kilichopo ni jambo la muhimu sana katika kipindi cha mwisho wa mwaka ili kuepuka kuwaweka watoto katika huzuni ya kushindwa kurejea shuleni

kwa wakati na kuepuka mashinikizo yanayoweza kusababisha kufanya uamuzi usio sahihi.

Nidhamu ya fedha katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka ni muhimu, hivyo tumalize mwaka kwa nidhamu katika matumizi ya fedha ili kuepuka fedheha ndogondogo zisizo za muhimu na zinazoweza kuepukwa. Nawatakia heri ya sikukuu na maandalizi mema ya mwaka mpya 2022 na kuwarejesha watoto shuleni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live