Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tsh. Bilioni 700 zinawekezwa Kilombero kukabiliana na uhaba wa Sukari

Sukari2 Tsh. Bilioni 700 zinawekezwa Kilombero kukabiliana na uhaba wa Sukari

Tue, 30 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMPUNI ya Sukari ya Kilombero, inatarajia kuanza mradi wake wa upanuzi ambao utakuza mchango katika ukuaji wa uchumi kutoka Sh. bilioni 340 za sasa hadi kufikia takribani Sh. bilioni 700 kwa mwaka.

Mradi huo wa upanuzi utakaohitaji uwekezaji mpya wa awali wa zaidi ya Sh. bilioni 550, unajumuisha kiwanda kipya kitakachokuza uwezo wa kampuni hiyo wa kutengeneza sukari na kupunguza uhaba nchini kupitia chapa yake ya “Bwana Sukari”.

Mkuu wa mauzo wa kampuni hiyo, Ephraim Mafuru, alibainisha hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika mkutano wa 20, wa taasisi za kifedha nchini.

Mafuru, alisema hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kampuni hiyo kufikia maono yake ya kupunguza utegemezi wa nchi katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa kuhakikisha kuwa inajitosheleza katika uzalishaji wa sukari ifikapo 2025.

“Mradi wetu wa upanuzi utakuza uzalishaji wa sukari kutoka tani 126,000 hadi tani 271,000 kwa mwaka hivyo kuisaidia serikali kuokoa takribani dola za Kimarekani milioni 70, katika uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi,” alisema Mafuru.

Mafuru aliongeza kuwa upanuzi huo unatarajiwa kukuza kiwango cha miwa kinachonunuliwa kutoka kwa wakulima ifikapo 2026/27 kwa takribani tani milioni moja kwa mwaka zaidi ya tani 600,000 zinazonunuliwa sasa na hivyo kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na uboreshaji wa miundombinu ya maendeleo na huduma za kijamii katika jamii zilizo jirani na kiwanda hicho.

Aidha, alisema kampuni ya sukari ya Kilombero imedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua uchumi ulioporomoka kutokana na janga la UVIKO-19.

“Pamoja na kukuza mchango wetu katika ukuaji wa uchumi, upanuzi huo utazalisha fursa za ajira za kudumu 2,000 na ajira 2,440 za mikataba, pamoja na kuzalisha Megawati 10 hadi 15 za umeme wa nishati mbadala zinazoweza kuingizwa kwenye gridi ya taifa kupitia mkataba wa ununuzi wa umeme (Power purchase agreement - PPA) na TANESCO,” alifafanua.

“Ujio wa UVIKO-19 kwa kiasi kikubwa umeyumbisha ukuaji wa uchumi kote duniani. Kiwanda chetu kipya kitawezesha kwa kiasi kikubwa kuunga mkono mkakati wa serikali wa kufufua uchumi, hasa kupitia ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa viwanda.

“Ni dhamira yetu kuendelea kuchangia katika kuboresha maisha ya jamii zinazotuzunguka na kukuza uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato ya wakulima, kuongeza mapato ya serikali, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, sambamba na kujenga thamani ya muda mrefu kwa wadau wetu wote,” alisema Mafuru.

Mradi huo wa upanuzi utanufaisha sekta mbalimbali, ukiwamo ujenzi, kilimo, viwanda na usafirishaji.

Kampuni ya sukari ya Kilombero, inamilikiwa na kampuni ya Illovo Sugar Africa kwa asilimia 75 na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 25.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live