Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tsh Bilioni 2.4/- kuboresha utalii wa malikale

F4a45c47c84e8bf18443764507ed8078 Sehemu ya hifadhi za malikale

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jumla ya Sh bilioni 2.4 zitatumika kuboresha sekta ya malikale katika vituo vya makumbusho nchini ili kukuza utalii na kuliingizia taifa mapato.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa uboreshaji wa Kijiji cha Makumbusho, kukuza utalii wa utamaduni kupitia Mpango wa Maendeleo wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid- 19.

Alisema fedha hizo ambazo zimetolewa na serikali, zitatekeleza miradi 15 katika vituo vya makumbusho ya taifa pamoja na kuboresha mazingira ya Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam kwa kujenga nyumba ya utamaduni ya kabila la Kizanaki na baadhi ya makabila mengine nchini.

"Kupitia fedha za Covid-19 serikali ilitoka Sh bilioni 2.4 kwa ajili ya kuboresha sekta ya malikale kutokana na kuathiriwa na janga la Covid -19, fedha hizi zitakwenda kutekeleza miradi 15 iliyopo katika vituo vyetu ambavyo ni Makumbusho ya Azimio la Arusha na Elimu Viumbe, Makumbusho ya Majimaji ya Songea na Makumbusho ya Mwalimu Nyerere Butiama na Malikale," alisema.

Aidha, alisema katika ya fedha hizo, Sh milioni 201 zimeelekezwa katika Kijiji cha Makumbusho kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbalimbali za asili za makabila kufuatana na ramani ya Tanzania pamoja na kukarabati miundombinu ya kiuhifadhi na kuboresha mandhari ya kijiji hicho.

"Ni matumaini yangu mradi huu ukikamilika katika kijiji hiki utakwenda kubadilisha sura na muonekano uliopo sasa na kuwa na muonekano mzuri ambao utasaidia kuongeza idadi ya watalii pamoja na kukuza mapato zaidi," alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Francis Michael aliwataka watumishi wa sekta hiyo kutumia vema fedha hizo na kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia.

Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Mawazo Ramadhani alisema miradi itakayotekelezwa katika eneo hilo ni kujenga nyumba za asili, ujenzi wa miundombinu ya kupambana na ajali za moto pamoja na kuboresha mandhari ya ndani na nje ya kijiji hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live