Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tsh. Bilioni 120 zimepatikana kwenye mavuno ya Ufuta

Zao Tsh. Bilioni 120 zimepatikana kwenye mavuno ya Ufuta

Mon, 20 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

WAKULIMA wa ufuta mkoani Lindi wamepata Sh. bilioni 120.6 baada ya kuuza kilo 49,885,228 za zao hilo kupitia mfumo wa stakabadhi gharani mwaka huu.

Takwimu hizo zilitolewa na Mshauri wa Kilimo na Rasilimali Watu, Majid Myao, wakati akiwasilisha taarifa ya mauzo ya zao hilo katika mkutano uliowakutanisha wadau wa zao hilo.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Myao alisema Mkoa wa Lindi uliweka malengo ya kuzalisha kilo 68,500,000 za ufuta, lakini kutokana na hali ya hewa kutokuwa nzuri na idadi ya ukubwa wa mashamba wamekusanya kilo 49,885,228 sawa na asilimia 72.8, hivyo kushindwa kufikia lengo lililokusudiwa.

Myao alisema mauzo na makusanyo ya ufuta huo ni kupitia minada 16 iliyofanywa na vyama vikuu vya ushirika vya Runali na Lindi Mwambao.

Alisema kutokana na kipato hicho, Sh.bilioni 8.8 ni makato ya ushuru yaliyopelekwa kwa wadau mbalimbali zikiwamo halmashauri za wilaya na manispaa kupitia mifuko ya elimu, kilimo, tari.

Myao alisema pia katika mgao huo Sh. bilioni 3.6 ni ushuru wa halmashauri zote sita ambazo ni Kilwa, Lindi Manispaa, Nachingwea, Mtama, Ruangwa na Liwale, wakati Sh. bilioni 1.2 zikipelekwa katika mfuko wa elimu ngazi ya wilaya na mkoa ukipatiwa mgao wa Sh. milioni 99.7 kila mmoja.

Alisema ugani na PYT Center ulipewa mgao wa Sh. milioni 99.7, Tari Sh. milioni 49.8, vyama vya msingi Sh. bilioni 2.9 wakati Sh.milioni 748.2 zikikadhiwa kwa vyama vikuu vya ushirika na Sh. bilioni 113.838 zimelipwa kwa wakulima.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Rajabu Telak, akizungumza na wadau hao wa kilimo, aliwasisitiza kutumia fedha walizolipwa kujiletea maendeleo, kwa kujenga bora na kusomesha watoto.

Chanzo: ippmedia.com