Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Trilioni nne zapeleka umeme vijijini

Umeme Ms Trilioni nne zapeleka umeme vijijini

Fri, 24 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) umetumia Sh4.35 trilioni kufikisha huduma za umeme kwa wananchi takribani milioni 40 wanaoishi katika vijiji 12,318 nchini, hivyo kuchechemua shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo.

Hata hivyo, tathmini ya Rea inaonyesha kwa ujumla, ni wastani wa asilimia 20 ya kaya katika kila kijiji, ndizo zimeunganishiwa umeme ikiwa ni chini ya asilimia 33 ya makadirio ya Rea ambayo ilianza utekelezaji wa majukumu yake miaka 15 iliyopita.

“Bajeti hiyo inahusisha vijiji vyote kufikishiwa umeme, tumeunganisha msongo wa kati wa kilovoti 33 kwa umbali wa kilometa 64,000,” amesema Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu, leo Novemba 23,2023 alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

Mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano ya tathmini ya kiutendaji ya mashirika ya umma inayoandaliwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambapo leo ilikuwa zamu ya Rea kueleza mafanikio, changamoto na mwelekeo mpya.

Katika wasilisho lake, Olotu amesema wakala huo pia umebakiza asilimia 55.74 ya vitongoji 64,760 kuunganisha huduma hiyo kwa mahitaji ya bajeti ya Sh67trilioni kabla ya mwaka 2030.

Katika ufafanuzi wake, Olotu amesema malengo ya kusambaza nishati hiyo vijiji ni kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, uhifadhi wa mazingira kupitia miradi ya nishati jadidifu na uboreshaji wa hali za maisha ya wananchi vijijini kupitia huduma za elimu na afya.

“Katika utekelezaji wa miradi hii, kuna mageuzi makubwa ya shughuli za kiuchumi na kijamii, kwa sasa kuna saluni za kunyoa, ajira za kuchomeleaji vyuma, viwanda vya kusaga na kukoboa, mabanda ya sinema na mipira, karakana za uchanaji mbao,”amesema Olotu.

Kwa mujibu wa takwimu za mwenendo wa hali ya shughuli za kiuchumi mwaka 2022, idadi ya waishio vijijini ni milioni 40.2 huku shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo zikiendelea kuchechemua ukuaji wa wastani wa pato la Taifa kwa kila Mtanzania kutoka dola 534 mwaka 2008 hadi dola 1,229.1 mwaka jana.

Olotu amesema awamu ya mradi wa majaribio mwaka 2008 ilifikia wilaya tano, awamu ya kwanza iliyoanza mwaka 2011 ikifikia vijiji 231, mradi wa Lindi na Mtwara vijijini 26, miradi midogo katika mikoa tisa ikifikia wateja wa awali 3,762, mradi wa Tazama na Mafia wateja 1,027 na awamu ya pili vijiji 2,948.

Pia miradi ya ujazilizi iliyofikia vijiji 295 na vitongoji 1,325, mradi wa Makambako-Songea vijiji 122, mradi wa Kiloviti 400(BTIP-VEI) vijiji 115, awamu ya tatu katika mzunguko wa pili vijiji 3,340, mradi wa pembezoni mwa miji maeneo 387, mradi wa nishati jadidifu vijiji 113 na miradi ya sola wilaya nane.

Kuhusu miradi ya nishati jadidifu, Mkurugenzi wa Teknolojia za nishati Jadidifu na mbadala kutoka Rea, Mhandisi Advera Mwijage amesema megawati 18 za umeme wa nishati jadidifu zimeunganishwa katika gridi ya Taifa, sawa na asilimia tano tu ya mchango wake.

Kwa mujibu wa Rea, majukumu mengine ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati safi katika visiwa 143 kati ya 196 vyenye makazi ya watu na uwezeshaji wa mikopo ya miradi ya ujasiriamali.

“Tunapeleka umeme jua visiwa 28 kwa Sh45 bilioni, Sh12 bilioni kwa mikopo ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini na Sh60bilioni ikihusisha mitungi ya LPG sh13bilioni, gesi asilia majumbani Sh24bilioni, majiko banifu Sh14bilioni na Sh10bilioni za miundombinu taasisi za umma,”amesema Adrera.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live