Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Treni yaleta ‘kilio’ usafiri wa mabasi Dar-Moshi

88204 Tren1+pic Treni yaleta ‘kilio’ usafiri wa mabasi Dar-Moshi

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kurejea kwa usafiri wa treni ya abiria kati ya Dar es Salaam na Moshi baada ya kupita miaka 25, kumetingisha usafiri wa mabasi kwenda mikoa ya kaskazini kutokana na idadi ya abiria kudaiwa kupungua.

Kwa kawaida kila mwishoni mwa mwaka huwa kuna mahitaji makubwa ya usafiri wa abiria wa kuelekea mikoa ya kaskazini ya Arusha na Kilimanjaro kutokana na watu wengi wenye asili ya huko kwenda kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya wakitokea sehemu mbalimbali nchini.

Wakati wadau wa usafiri wa mabasi na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) wakikiri abiria kupungua tangu treni ilipoanza kutoa huduma Ijumaa iliyopita, uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) umeongeza safari za treni kutoka mbili kwa wiki hadi tatu kutokana na wingi wa abiria.

Treni hiyo ilianza kutoa huduma Ijumaa iliyopita ikiwa na mabehewa nane (saba ya abiria) kwa kuondoka Dar es Salaam saa 10 jioni na kuwasili Moshi, Jumamosi iliyopita saa 5 asubuhi na iliondoka siku hiyohiyo mjini Moshi saa 10 jioni kurejea Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hali ya usafiri wa mabasi kwenda mikoa ya kaskazini kwa sasa katibu wa Taboa, Enea Mrutu alisema “usafiri wa treni umetukata koo kwa kweli abiria hakuna kama siyo mwezi Desemba? Yaani nyakati kama hizi unakuta mabasi ya kwenda Arusha na Kilimanjaro mchana? Ajabu miaka iliyopita huwezi kukuta jambo hili.”

Mawakala wa mabasi waliozungumza na Mwananchi nao walieleza changamoto hiyo, huku abiria wa treni wakieleza jinsi usafiri huo ulivyo na nauli nafuu kuliko ile ya basi na umesaidia kupunguza gharama kwa wanaosafiri kama familia na pia kuwepo fursa ya kubeba mizigo mingi.

Awali, TRC ilieleza kuwa treni itakuwa inatoka Dar es Salaam Ijumaa na Jumanne na Moshi-Dar es Salaam kila Jumatano na Jumamosi. Ratiba hiyo ilidumu kwa simu mbili tu kwani kuanzia Jumatatu wiki hii, safari zimeongezwa hadi tatu kwa wiki.

Siku ya kwanza treni hiyo iliondoka Dar es Salaam ikiwa na abiria 263 wakati 24 walipandia njiani. Ilitoka Moshi kwenda Dar es Salaam ikiwa na abiria 241.

Idadi hiyo ya abiria wa treni kwa safari moja ni takribani mabasi sita ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 35 hadi 58.

Treni hiyo ambayo imeongezwa mabehewa ya abiria kutoka saba hadi nane kuanzia Jumatatu iliyopita, ina madaraja matatu.

Behewa la daraja la tatu lina uwezo wa kupakia abiria 80 waliokaa, daraja la pili kukaa abiria 60 na daraja la pili kulala abiria 36 huku nauli ikiwa Sh16,500 (daraja la tatu), Sh23,500 (daraja la pili kukaa) na Sh39,100 daraja la pili kulala.

“Hali ya usafiri wa mabasi imekuwa ngumu, treni imetupunguzia abiria, ukweli ndio huo. Mwaka jana mwezi Desemba mchana huwezi kukuta basi la kwenda Moshi au Arusha, ila sasa yapo,” alisema Mohammed Papaa, wakala wa mabasi kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo.

“Kulikuwa na tabia ya kupandisha nauli za mabasi Desemba, lakini sasa abiria hawaonekani wamekimbilia kwenye treni unapandishaje?” alieleza Papaa.

Wakala mwingine kituoni hapo, Mathias Mrema alitahadharisha hali hiyo ikiendelea, huenda baadhi ya matajiri wakabadilisha biashara na kuhamia katika shughuli nyingine kwa kuwa hawatapenda kuona wakipata hasara.

“Sasa hivi abiria unawaona kuanzia saa moja asubuhi tu, baada ya hapa hakuna kitu,” alisema.

Aisha Miraj, mjasiriamali katika kituo cha Ubungo alisema tangu kuanza kwa treni hiyo abiria, wamepungua.

“Biashara zetu haziendi vizuri kwa kuwa abiria wamepungua,” alisema Miraj.

Mjumbe wa Taboa, Mustapha Mwalongo alisema licha ya abiria kupungua, uwepo wa usafiri wa treni umewapa unafuu kwa kuwa miaka iliyopita kipindi kama hiki walikuwa wakitafuta mabasi kwa ajili ya kupunguza abiria.

“Maendeleo yoyote hayakosi changamoto. Haya ni maendeleo kwa serikali, lakini ni changamoto kwa wadau wa usafiri wa mabasi kwa sababu abiria wamepungua,” alieleza.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akielekea Arusha, Said Ally alisema, “Treni imesaidia kupunguza changamoto ya usafiri hapa Ubungo hasa kipindi cha mwisho wa mwaka. Sasa hivi unachagua usafiri na treni au basi.”

Abiria wa treni, Tongeni Mzava alisema, “leo (jana) nipo Dar es Salaam kufanya biashara zangu naondoka jioni na usiku nitalala kwenye treni na kufika Moshi asubuhi na kuendelea na biashara zangu. Katika treni uko huru zaidi, unakwenda maliwatoni, chakula unapata kwa wakati, unalala na kuamka muda unaopenda, ni usafiri mzuri.”

Maysara Mfinanga alisema, “huwa nasafiri kwa wasiwasi na basi, kwanza mwendo kasi lakini kwenye treni una uhakika utafika. Kwenye treni unaweza kulala, kukaa kama mimi hakuna shida kabisa.”

Naye Flora Akwilapo alisema, “siku za nyuma nilikuwa nasafiri na mabasi ila ilikuwa usumbufu unakaa saa nane kwenye basi mgongo unauma ila katika treni hali ni nzuri zaidi.”

Kauli ya TRC

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano TRC, Jamila Mbarouk alisema wamelazimika kuongeza safari tatu kutoka mbili kutokana na wingi wa abiria.

“Kutokana na mahitaji ya abiria kuanzia Jumatatu ijayo tumeongeza safari, itakuwa inaondoka Dar es Salaam Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na kuondoka Moshi kuja Dar es Salaam kila Jumanne, Alhamisi na Jumamosi.”

“Mahitaji ya abiria yamekuwa makubwa kwa hiyo tumeongeza siku za kusafiri,” alisema na kueleza pia wameongeza mabehewa ya abiria kutoka saba hadi nane.

Hata hivyo, jana asubuhi zilienea taarifa mitandaoni zikidai kuwa treni hiyo imejaa hadi Desemba 27, kitu ambacho kimekanushwa na Mbarouk.

Alisema, “Sisi huwa tunakatisha tiketi siku tatu kabla ya safari, hivyo kusema kuwa nafasi zimejaa hadi Desemba 27 ni uongo si taarifa za kweli na wasafiri wapuuze habari hizo. Ila ninachoweza kukuthibitishia ni kuwa abiria wanaongezeka kwa kasi kila siku ya safari.”

Chanzo: mwananchi.co.tz