Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema wanatarajia kuanza rasmi safari za reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ya kilometa 300 kati ya Dar es Salaam na Morogoro kuanzia Februari 2023.
Kadogosa ameyasema katika hafla utiaji saini wa mkataba wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 51 kati ya TRC na kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology (SSRST) kutoka nchini Korea Kusini iliyofanyika jana Jumatatu, Novemba 7, 2022 jijini Dar es Salaam.
Amesema hatua hiyo itafikiwa baada ya kukamilika kufanyika kwa majaribio na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kujiridhisha.
Kuhusu gharama za nauli ya kusafiri na treni hiyo, Kadogosa amesema zitatolewa baada ya taratibu kukamilika lakini wananchi watarajie kuwa zitakuwa nafuu ambazo hata mwananchi wa kipato cha kawaida anaweza kumudu.
“Suala la bei lina taratibu zake sio la kujifungia ndani na kutoa bei, tunatakiwa kuzunguka mikoa mbalimbali kuzungumza na wananchi na wadau mbalimbali hadi pale tutakapokubaliana kama taifa,” amesema.
Kuhusu mkataba uliosainiwa, Kadogosa amesema unagharimu dola za Kimarekani dola milioni 51 kwa ajili ya kununua machine na mitambo 26 matengenezo ya njia ya reli ya kisasa (SGR) na utekelezaji wa mkataba huu ambao utahusisha utengenezaji, mafunzo, makubaliano na makabidhiano unatarajiwa kufanyika kwa miezi 12.
Amesema lengo la ununuzi wa mashine na mitambo hiyo ni kuongeza ufanisi wa matengenezo ya njia na kupunguza kufanya matengenezo ya njia kwa kutumia watu.
"Mitambo hiyo itaipa uwezo TRC katika kutunza njia ya SGR muda wote wa uendeshaji na utahusisha ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwemo mashine ya ukaguzi wa njia, mtambo wa kukagua mipasuko ya ndani ya reli, mtambo wa kuzima moto sehemu mbalimbali za reli ikiwemo mahandaki na nyinginezo," ameasema.
Pia, amesema sambamba na ununuzi huo, TRC tayari imeandaa wafanyakazi watakaofundishwa namna bora ya kutumia mashine na mitambo hiyo kwa ufanisi.
Naye Makamu wa Rais wa kampuni ya SSRST, Charles Park amesema ufanisi wa utekelezaji wa mkataba huo unahitaji ushirikiano baina ya TRC na SSRST.
Kwa upande wake balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania, Kim Sun Pyo amesema mkataba huo unaendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi ya Tanzania na Korea Kusini