Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tozo za Uvuvi zaboreshwa

C3ca5f8389daa0c4f4968cd28ab2b21d Wizara ya Uvuvi imeboresha na kuondoa baadhi ya tozo kwa wavuvi nchini

Fri, 5 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dk Rashid Tamatamah, amesema tozo nyingi katika sekta ya uvuvi ambazo zipo chini ya wizara tayari zimeboreshwa na nyingine kuondolewa ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kufanya kazi kwa wadau wa uvuvi nchini.

Dk Tamatamah amesema hayo leo katika Mwalo wa Ihale uliopo Wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu, wakati akikagua ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mwalo huo.

Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wizara zingine pamoja na halmashauri za wilaya kote nchini zinaendelea kuangalia tozo za uvuvi ambazo siyo rafiki kwa wadau wa uvuvi.

Amesema nia ya serikali ni kuondoa vikwazo vya biashara na utekelezaji wa agizo kutoka katika mamlaka ya juu ya serikali katika mwaka huu wa fedha 2021/22 wa kuondoa tozo ambazo zinakwamisha maendeleoa ya sekta mbalimbali nchini.

“Rais Samia Suluhu, aliagiza wizara zote ziangalie upya tozo ambazo katika kila sekta zipo kwa kushirikiana na halmashauri kwa mfano sisi wizara ambazo zipo chini ya wizara nyingi tumezipunguza, kila tunapopita katika halmashauri tunawaambia pamoja na wizara zingine juu ya tozo zinazohusu sekta ya uvuvi.” amesema Dk. Tamatamah

Katibu mkuu huyo amebainisha hayo baada ya kukutana na baadhi ya wadau wa uvuvi katika Mwalo wa Ihale na kujulishwa juu ya tozo mbalimbali za sekta ya uvuvi ambazo wanaona zimekuwa zikiwakwamisha kufanya biashara.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Busega, Gabriel Zacharia alizungumzia juu ya uwepo wa tozo ambazo wadau wa uvuvi wamekuwa wakizilalamikia ikiwemo ambayo inatozwa kwa thamani ya dola za kimarekani.

Aidha, Zacharia ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kubainisha kuwa kumekuwa hakuna malalamiko makubwa kutoka kwa wadau wa uvuvi juu ya mambo mengine ambayo sekta ya uvuvi inahusishwa ukizingatia Wilaya ya Busega ndiyo wilaya pekee katika Mkoa wa Simiyu ambayo ina sehemu ya Ziwa Victoria.

Wakati huo huo, Tamatamah amefanya ukaguzi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Kituo cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kanda ya Simiyu na Magu lililopo Kasadima na ujenzi wa Mwalo wa Ihale katika ya Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, amesema ameridhishwa na ujenzi unavyoendelea huku akiwataka makandarasi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 Mwaka 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz