Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde amesema anafarijika kuona namna sekta binafsi zinavyoshiriki kukuza ujuzi kwa vijana utakaowasaidia kujiajiri wenyewe.
Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, alitoa kauli jana usiku Machi 5, 2019 katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa shindano linalowalenga vijana wenye mawazo mbadala ya biashara na miradi inayoweza kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii linaloitwa “Startupper of the Year Challenge”.
Shindano hilo limeandaliwa na kampuni ya Mafuta ya Total lenye lengo la kuwawezesha kimitaji wajasiriamali wadogo wenye mawazo mazuri ya kibiashara yatakayosaidia Taifa na jamii katika kuleta maendeleo.
Mavunde amesema hatua hiyo ni muhimu hasa katika nyakati hizi za kujenga uchumi imara utakaoimaraisha nguvu kazi na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo kusudi kuleta maendeleo kwa vijana.
“Ili tufikie malengo ya nchi ya kipato cha kati, ni lazima tuijengee uwezo nguvu kazi yetu. Ndiyo maana Serikali inaendesha mpango wa kukuza ujuzi wenye lengo la kuwafikia Watanzania milioni 4.4 ifikapo mwaka 2021,” amesema Mavunde.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Total, Tarik Moufaddal alisema shindano la kwanza lilifanyika mwaka 2015 na mchakato huo unazingatia wazo la ubunifu umuhimu wa mradi huo kwa jamii na kuendelea kwa mradi huo katika kuleta maendeleo
“Katika shindano hili la awamu ya pili mshindi wa kwanza atapata Sh 30milioni, wa pili Sh 20 milioni na Sh 15milioni,”amesema Moudaffadal.
Katika shindano hilo jumla wa washiriki 600 walijitokeza kuandika miradi yao ya ubunifu lakini Doreen Peter Noni aliibuka kidedea, akifuatiwa na Sai Michael na Prince Tilya.