Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) yazitaka kampuni za bima nchini kuvumbua bidhaa mbalimbali ambazo zinaendana na mahitaji ya soko, ikiwa ni pamoja na kuzifikia sekta ya mifugo na misitu.
Hayo yamebainishwa jana na Kamishna wa mamlaka hiyo, Dk Baghayo Saqware, wakati wa uzinduzi wa bima ya kilimo ijulikanayo kama Mtetezi inayolenga kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.
“Strategis ni moja ya kampuni zinazowekeza katika uvumbuzi wa bidhaa zinazokwenda na mahitaji ya soko. Nakumbuka miezi miwili iliyopita, kampuni hii ilizindua bima ya container insurance,” amesema Dk Saqware.
Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji wa soko la bima nchini, mauzo ya bima ya kilimo ilikuwa Sh1.3 bilioni 2021 ikiwa ni asilimia 0.17 ya mauzo yote ya bima za kawaida ambaso kimsingi zilizofikia Sh746.6 bilioni mwaka huo.
Tira inafafanua katika taarifa hiyo kuwa ongezeko hilo dogo linatokana na sababu kadhaa ikiwemo ya kutopatikana kwa taarifa za kutosha kuhusu bima ya kilimo, kukosekana kwa skimu ya bima ya kilimo na uwepo teknolojia ndogo ya miundombinu kwa bima za kilimo.
Hivyo basi, Dk Saqware amewaomba Strategis kuangalia uwezekano wa kutoa bidhaa nyingine za bima kwenye upande wa mifugo na misitu zitakazo kuhakikisha wakulima wanaongeza uzalishaji wa mazao pamoja na kukabiliana na majanga yakiwamo yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini.
Taarifa kutoka Wizara ya Kilimo zinabainisha kuwa kilimo ni biashara yenye vihatarishi vingi vinavyosababishwa na utegemezi wa mvua, mabadiliko ya hali ya hewa, moto, uharibifu wa ndege na
Hivyo, kuanzishwa kwa huduma za bima kwenye kilimo ni hatua muhimu kwa wakulima nchini Tanzania ili kukabiliana na hasara zitokanazo na vihatarishi vinavyoathiri uzalishaji.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Strategis, Dk Flora Minja amesema kampuni hiyo inaamini kuna nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Amesema uwekezaji na mipango iliyofanyika na inayoendelea kufanyika, imewapa wadau matumaini ya sekta hiyo kuendelea kukua zaidi.
“Bima hii mpya itawalinda wakulima dhidi ya majanga mbalimbali yanayoathiri mavuno ya mazao. Wakulima watapata fidia endapo watakumbana na majanga yanayoweza kuathiri mavuno yao kama vile hali ya hewa, wadudu, magonjwa na majanga mengine,” amesema Dk Flora.
Akitoa maelezo kuhusu huduma hiyo, Ofisa Mkuu Mtendaji wa Strategis upande wa bima za mali na ajali, Jabir Kigoda amesema bima ya Mtetezi ina faida kwa wakulima na wadau wote katika sekta ya kilimo.
“Huduma hii ya bima inatoa kinga ili kuhakikisha mkulima anapata mavuno anayostahili kutoka eneo lake husika kwa kuangalia historia ya uzalishaji wa eneo hilo,” amesema Kigoda.
Kigoda amesema wameona juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya kilimo.
“Kumekuwa na mikakati mizuri sana ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali na kuwapa matumaini wananchi. Hata hivyo, wakati tunafurahia jitihada hizi, ni lazima tujue kuna majanga yanayoweza kuja na kuharibu uwekezaji huo uliofanywa kwenye sekta hii. Tunaamini, bima ya kilimo ya Mtetezi itakuja kulinda uwekezaji huo uliofanywa,” amesema Kigoda.