Imeelezwa kuwa wastani wa asilimia 14 ya ardhi inayotumika kwa kilimo Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, imeathirika kwa kiwango kikubwa cha tindikali na kusababisha uzalishaji wa mazao ya chakula kushuka na wakulima kutozalisha kwa tija.
Mtafiti wa afya ya udongo kutoka Taasisi ya utafiti wa kolimo nchini (Tari ) kituo cha uyole , Fredrick Mlowe ametoa taarifa hiyo leo Jumatatu, Mei 15,2023 kwenye mkutano wa wadau uliolenga kuwasilisha taarifa ya ugunduzi wa chokaa kutumika kudhibiti wingi wa tindikali ardhini.
Mkutano huo umeshirikisha wataalam wa utafiti wa kilimo kutoka TARI, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Maofisa kutoka katika Kiwanda cha Saruji cha Mbeya (Mbeya Ciment), ambacho kitazalisha chokaa na kusambaza kwa wakulima .
Amesema uwepo wa tindikali kwenye ardhi umechangia kushuka kwa uzalishaji, kutokana na mazao yanayolimwa kushindwa kufyonza virutubisho vinavyowekwa kwa ajili ya kunenepesha mimea.
“Tafiti zilizofanywa zinaonyesha kati ekari moja ya shamba la mahindi, mkulima anatakiwa kuvuna wastani wa zaidi ya tani tatu, lakini kutokana na changamoto hiyo, Mikoa yetu imeshindwa kuzalisha kutokana na wingi wa tindikali ardhini,” amesema.
Amesema kutokana na changamoto hiyo wamelazimika kukutana kujadiliana na kupata mwarobaini ambao ni matumizi ya chokaa ambayo wakulima wanashauriwa kutumia na kwamba ina uwezo wa kufyonza sumu kutokana na uwepo wa madini yenye uwezo wa kuondoa tindikali hizo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tari-Uyole, Dk Juliana Mwakasendo amesema baada ya kubaini kuwepo na wingi wa tindikali na kupata mwarobaini wameanza kuhamasisha wananchi kutumia chokaa ili kupunguza madhara na kutozalisha mazao yenye tija na kufikia malengo.
“Teknolojia ya kutumia chokaa ni muhimu, hasa ikitumika ipaswavyo inasaidia kupunguza tatizo hilo na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula,” amesema.
Amesema mikakati mingine kutoa elimu ya matumizi ya chokaa kwa wakulima mikoa ya nyanda za juu kusini na kusambaza kupitia kiwanda cha saruji Mbeya ambao wamekubali kuwafikia wakulima.
“Tayari tumezungumza na uongozi wa kiwanda cha Saruji Mbeya - Mbeya Cement, kwa ajili ya kuzalisha chokaa kwa wingi na kuwafikishia wakulima, ambao watatumia katika uzalishaji wa mazao yenye tija” amesema.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Saruji, Khaled Ghareob amesema watahakikisha wanazalisha chokaa ya kutosha na kuisambaza kwa wakulima ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta ya kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffari Haniu, amesisitiza wakulima kutumia teknolojia hiyo ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na kudhibiti tindikali iliyoathiri afya ya udongo.
“Ikumbukwe rasirimali ya chokaa sio kwa ajili ya kujengea nyumba tu, Tari wamebaini ina uwezo wa kudhibiti tindikali zanye sumu zinazodaiwa kuathiri asilimia kubwa ya udongo unaotumiwa kwa kilimo Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,” amesema.
Mkulima Witness John amesema wamepokea hoja hiyo ya utafiti uliofanywa kikubwa wanaomba elimu itolewe ili waweze kwenda na wanati na kurejesha ubora wa udongo.