Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thamani za miamala simu yashuka, wasomi wanena

Thamanipiichnhnh Thamani za miamala simu yashuka, wasomi wanena

Fri, 28 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Wakati idadi ya watumiaji wa huduma za fedha kwa simu za mkononi ikizidi kuongezeka, thamani ya miamala wanayoifanya inapungua kila uchao.

Ripoti ya robo mwaka inayoishia Septemba 2022 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha idadi ya miamala imeongezeka kutoka zaidi ya milioni 349.9 iliyofanywa Julai mpaka milioni 366.2 ya Septemba. Kwa Agosti, ilifanyika milioni 356.8.

Miamala hiyo, ripoti inasema thamani yake ilipungua kwa miezi mitatu mfululizo. Kwa Julai kila muamala uliofanywa ulikuwa na wastani wa thamani ya Sh35,857 ambayo ilishuka mpaka Sh35,710 kwa Agosti na Sh34,742 kwa Septemba thamani ilikuwa Sh34,742.

Mtafiti na Mhadhiri Mwandaimizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi ameeleza kushuka kwa thamani ya miamala hiyo kunasababishwa na wingi wa tozo, hivyo watu kuanza kukwepa kutumia njia hiyo kufanikisha miamala waliyoikusudia.

“Hii (uwepo wa tozo) ilisababisha baadhi ya watu waliokuwa wakifanya miamala kuacha na kuamua kutumia njia mbadala ya kupeleka fedha kwa kutumia usafiri ili wakwepe gharama,” alisema.

Kuhusu athari za kiuchumi zinazoweza kutokea kutokana na kushuka kwa thamani ya miamala hiyo ya simu, alisema kutapunguza mapato ya Serikali yatokanayo na kodi na tozo zilizopo kwenye eneo hilo, kwani wingi wake, pamoja na mambo mengine, hutegemea thamani ya huduma iliyotolewa.

“Matumizi yanapungua hivyo mapato yatapungua pia, kwa kuwa watu wanatumia njia mbadala, kitu ambacho kinaweza kuchochea kupungua kwa fedha kwenye mfumo rasmi,” alisema.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, Profesa Abel Kinyondo alisema tofauti ya thamani ya miamala hiyo ni ndogo, hivyo athari zake zinaweza zisionekane kirahisi.

“Tunatakiwa kutambua kuwa kushuka kwa thamani ya miamala, kama imepungua kutoka wastani wa Sh35,000 hadi Sh34,000 sio kubwa sana zinazoweza kutuumiza,” alisema.

Hata hivyo, Profesa Kinyondo ameshauri kuwapo kwa ushirikishaji wa huduma za fedha ili kuwawezesha watu kufanya miamala kielektroniki.

Nini kifanyike

Kutokana na mwenendo wa thamani ya miamala hiyo kushuka, Profesa Moshi alisema anategemea Serikali itafikiria kupunguza tozo kwa kuwa dunia inahamia kwenye uchumi wa kidijitali na Watanzania hawawezi kuuepuka, hivyo gharama za miamala hiyo zinapaswa kuwa chini kadiri iwezekanavyo.

“Watu wanatakiwa kutambua tunapokwenda kwenye uchumi wa kidijitali Serikali inapaswa kuhakikisha haileti vitu vinavyosababisha watu kukwepa kuzitumia huduma zinazofanikisha miamala hiyo,” alishauri.

Profesa Kinyondo naye alisema kuna haja ya kutatua mapema changamoto zilizopo kabla tatizo halijawa kubwa kiasi cha kuathiri uchumi.

“Takwimu za TCRA katika miezi mitatu sio mwenendo mzuri na unatakiwa kutatuliwa kabla ya tatizo kuwa kubwa, kwa sasa sio kitu kikubwa sana kuchukua kwa sababu katika uchumi mpaka madhara yatokee lazima kitu kiwe na takwimu muhimu (achano kubwa),” alishauri.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Haji Semboja alisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kuwa na timu ya kushauri masuala ya kiuchumi.

“Kama wanataka fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, wanatakiwa kushauriana na watu wenye uelewa na hivyo vitu ili waweze kuwaonyesha, tukifanya hivi tutafika sehemu fulani,” alisema.

Hata hivyo, ripoti hiyo inakuja ikiwa ni wiki nne tangu Serikali itangaze viwango vipya vya tozo vya miamala ya kielektroniki inayojumuisha ile inayofanywa katika simu hata kwenye akaunti ya benki baada ya malalamiko ya wananchi kuhusu viwango vilivyokuwapo awali.

Chanzo: mwanachidigital