Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thamani uwekezaji yazidi kupaa

Materu3 Thamani uwekezaji yazidi kupaa

Mon, 31 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema kiwango cha uwekezaji, thamani na kiasi cha ajira katika miradi inayoanzishwa vinazidi kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Pwani, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hatua hiyo ni tija kwa taifa.

Msigwa alsema serikali imekuwa ikiboresha mazingira ya uwekezaji nchini kwa kusikiliza changamoto za wawekezaji na kuzipatia ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kuondoa urasimu, na kurahisisha utoaji wa vibali muhimu na kwamba hatua hizo zimechangia wawekezaji wengi kujenga imani na kuwekeza.

Alisema kwa mwaka jana miradi 222 ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yenye thamani ya Sh trilioni 6.1 wakati kipindi kama hicho mwaka 2020 miradi iliyosajiliwa ilikuwa 173 yenye thamani ya Sh trilioni 2.1

Msigwa alisema miradi iliyosajiliwa mwaka jana ilizalisha ajira zaidi ya 49,944 wakati miradi ya mwaka 2020 ilizalisha ajira 14,819.

Alisema katika miradi iliyosajiliwa mwaka jana 66 ni ya wazawa na 60 ni ya ubia.

Kuhusu mkongo wa taifa, Msigwa alisema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 600 na unatarajiwa kutekelezwa kwa umbali wa kilomita 15,000 na hadi sasa mkongo huo umefika kilometa 8,119.

Alisema hivi sasa utekelezaji mwingine wa kilomita 4,442 unaendelea mwaka huu na kusema utekelezaji wake unaendelea huku pia maboresho ya uwezo wa mkongo yakifanywa kutoka uwezo wa G 2 hadi G8.

Alisema mkongo huo unaendelea kusambazwa pia kwenye nchi Jirani na hivi sasa unapelekwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kwamba faida ya nchi kupeleka mkongo huo huku ni kupata fedha kwa sababu wanaotumia wanalipia huduma hiyo.

Aidha alizungumzia kupanda kwa bei ya vyakula nchini na kusema serikali haijapandisha bei na badala yake imadhibiti kusiwemo na mfukumo wa bei ili wananchi wake wasipate taabu.

Alisema kupanda kwa bei vya vyakula na bidhaa ngingine kunatokana na janga la corona duniani ambalo limeathiri uzalishaji kwenye viwanda vingi na baadhi kufunga au kupunguza uzalishaji na hali itatengemaa pale janga hilo litakapopungua au kutokomea.

Akizungumzia hali ya corona nchini, Msigwa alisema ugonjwa huo badi upo na kuwataka watanzania kuendelea kuchukua hadhari na kuchanja.

Alisema hadi sasa jumla ya dozi milioni 8.82 zimeingia nchini na vituo vyote vya kutolea huduma hiyo vina chanjo.

Kuhusu sensa ya watu na makazi, Msigwa alisema itafanywa Agosti mwaka huu Tanzania Bara na visiwani sambamba na uboreshaji wa anuani za makazi na kuwataka wananchi kujitokeza wakati za sensa ili kuhesabiwa na serikali ipate idadi kamili ya watu wake iweze kuwahudumia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live