Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Thamani uwekezaji masoko ya mitaji yafika Sh32.7 trilioni

Mtajipiic Data.png Ofisa tendaji mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: mwananchi Digital

Thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 12.02 na kufikia Sh32.7 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2022 ikilinganishwa na Sh29 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Machi 24,  2022 na ofisa mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama alipokuwa akizungumzia mafanikio ya mwaka mmoja wa uongozi wa  Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.

Mkama amesema mafaniko hayo ya kukua kwa masoko ya mitaji yametokana na sababu mbalimbali kubwa ikiwemo mazingira wezeshi, shirikishi na endelevu ya kisera, kisheria na kiutendaji ya Serikali.

“Ni katika mafanikio haya jumla ya mauzo ya hisa na hatifungani yameongezeka kwa asilimia 19.2 na kufikia Shtrilioni 3.1 katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na Sh2.6 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2021.

“Wakati mauzo ya hatifungani za Serikali yameongezeka kwa asilimia 38.1 na kufikia Sh2.9 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2022, ikilinganishwa na Sh2 trilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2021."

“Huku thamani ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja katika kipindi kilichoishia Februari 2022 imeongezeka kwa asilimia 55.8 na kufikia Sh868 bilioni ikilinganishwa na Sh 557 bilioni katika kipindi kilichoishia Februari 2021,”amebainisha Mkurugenzi huyo.

Advertisement Amesema mpaka sasa masoko ya mitaji Tanzania ni miongoni mwa masoko matano bora yaliyopata mafanikio makubwa kiutendaji barani Afrika ndani ya kipindi hiko cha mwaka mmoja.

Amebainisha kuwa mamlaka imetekeleza mikakati ambayo imewezesha kufungua nyanja mpya katika masoko ya mitaji ambayo ni  kuanzisha bidhaa na huduma mpya, bunifu, zenye mlengo maalum na matokeo chanya kwa jamii.

Mikakati mingine ameitaja kuwa ni  matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kutoa huduma, kuongeza idadi ya wataalamu wanaokidhi viwango vya kimataifa na kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji.

Ameeleza kuwa katika kuboresha utendaji wa soko la hisa, mamlaka imeidhinisha mabadiliko ya kanuni za soko la hisa la Dar es Salaam ili kuwezesha utoaji na uorodheshwaji wa bidhaa mpya, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazolenga kugharamia miradi ya maendeleo inayochangia utunzaji wa mazingira, maendeleo ya jamii na utawala bora.

Chanzo: mwananchi Digital