THAMANI ya mali za Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), zilizokaguliwa zimeongezeka mara nne zaidi katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kutoka Sh. trilioni 1.4 mwaka 2010 hadi Sh. trilioni 4.98 mwaka 2020.
Taarifa ya NHC inaonyesha kuwa thamani hiyo ya mali zinazohamishika na zisizohamishika ni kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Thamani hii ni sawa na ukuaji wa zaidi ya asilimia 255.7 ya mali za shirika ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.
“Thamani hiyo inahusisha vitegauchumi vya majengo na ardhi ghafi inayomilikiwa na NHC ambayo bado haijaendelezwa, ikiwa ni pamoja na miradi ya nyumba inayoendelea.”
Taarifa ya tathmini ya mwenendo wa shirika hilo imesema licha ya kupanuka kwa malengo yake na kuwapo kwa miradi mikubwa zaidi, NHC bado inatimiza lengo lake la awali la kutoa makazi bora kwa watu wa kipato cha chini.
“Licha ya mabadiliko mengi, lengo la msingi la shirika bado lipo. Tulilazimika kupanua malengo kwa kuongeza miradi mikubwa ili kupata pesa za kujiendesha na kuendelea kudumu kwenye soko,” amefafanua Muungano Saguya, Meneja Uhusiano na Habari wa Shirika hilo.
Pamoja na miradi mikubwa kama vile Morocco Square jijini Dar es Salaam na mingine, bado NHC imeendelea na miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kupangisha na kuuza kwa wahitaji.
Alifafanua kuwa baada ya miaka mingi ya kutoa huduma tangu kuanzishwa kwake mwaka 1962, NHC ilielekezwa kisheria kuanza kujiendesha kibiashara kuanzia mwaka 2005.
Hadi kufikia Juni 2021 shirika lilikuwa linatekeleza miradi nane katika hatua mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na mitatu ya nyumba za gharama nafuu na mitano ya nyumba za gharama za kati za juu na majengo ya biashara na ofisi.
Miradi ya ujenzi inayoendelea ni ya gharama nafuu ya Igunga, Makete na Iyumbu, pamoja na miradi ya gharama ya kati na juu ya Morroco Square, Kawe, Regent Estate na mradi wa Chamwino.
Alisema NHC imelazimika kuomba serikalini kibali cha kukopa kiasi cha Sh. bilioni 173.9 ili kukamilisha miradi inayoendelea ya gharama ya juu jijini Dar es Salaam.