Thamani ya bidhaa zilizoteketea kwa moto kwenye ghala lililopo kwenye bandari ya Tanga linalomilikiwa na Mamlaka ya mapato Tanzania 'TRA' mkoani humo kuhifadhia bidhaa za magendo zilizokamatwa na zilizoshindwa kulipiwa ushuru imejumlishwa na kufikia zaidi ya milioni mia tano.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba ametoa kauli hiyo ofisini kwake wakati akiwa na waandishi wa habari mara baada ya kuunda kamati ya watu 11 kwaajili ya kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto huo uliosababisha hasara kwa mali zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya ghala hilo.
"Thamani inayokadiriwa kutokana na thamani iliyopo kwenye nyaraka ambayo sio thamani ya soko ni zaidi ya shilingi milioni 541 ambayo kodi yake ni zaidi ya milioni 423 hii ni thamani ya bei ambayo imeandikwa kwenye nyaraka ndiyo tumeichukuwa " alisema Mgumba.
Mgumba amesema kuwa kamati hiyo itachukuwa siku saba kutafuta chanzo cha moto huo na miongoni mwa watu watakaohojiwa ni pamoja na mtumishi wa mamlaka ya mapato Tanzania Mkoa wa Tanga aliyemtaja kwa jina moja la Kisaka ambaye ambaye yupo kwenye kamati maalumu ya kupambana na bidhaa kwa kushindwa kutoa ushirikiano wakati tukio hilo likiendelea hata alipopigiwa simu yake ya kiganjani hakutoa ushirikiano wowote.