Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Televisheni, redio zabanwa matangazo mubashara

2c84b97591d7693e85411a327ae3bd55 Televisheni, redio zabanwa matangazo mubashara

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mwongozo mpya unaovitaka vituo vya utangazaji kutoa taarifa kwa mamlaka hiyo kabla ya kurusha matangazo yoyote mubashara.

Akizungumza katika kikao cha mtandao baina ya TCRA na watoa huduma wenye leseni ya huduma ya maudhui, Mkurugenzi wa Leseni TCRA, Andrew Kisaka alisema mwongozo huo uliotolewa Machi 18, mwaka huu unazingatia mwongozo uliotolewa Septemba 7, mwaka jana.

“Vituo vya utangazaji vitatakiwa kufuata mwongozo huu mpya ulitolewa na TCRA kabla ya kutangaza matukio mubashara na mwongozo huu umelenga maeneo matatu muhimu,” alisema Kisaka.

Alisema vituo hivyo vitatakiwa kutoa taarifa ya kimaandishi kwa mamlaka hiyo siku 14 kabla ya kurusha mubashara matukio ya kitaifa yaliyopo kwenye kalenda ya mwaka.

Kisaka alisema kituo kitatakiwa kutoa taarifa ya maandishi siku moja kabla ya kurusha mubashara matangazo ya dharura ambayo hayako kwenye kalenda na kutaja baadhi ya matukio hayo kuwa ni ziara za viongozi na uzinduzi wa miradi.

Aidha, alisema pia mwongozo huo unavitaka vituo hivyo kutoa taarifa TCRA siku moja kabla ya kurusha matangazo ya mubashara ya matukio muhimu ya kijamii kama vile mashindano ya michezo ya mpira, matukio muhimu ya viongozi wa kiserikali au sherehe za kidini.

“Kwa mujibu wa mwongozo huu katika kila taarifa ya kituo lazima ianishe tukio litakalotangazwa, mahali tukio litakapofanyika na muda wa kuanza na kumalizika kwa tukio,” alisema Kisaka.

Aliongeza, “Kituo cha utangazaji hakiruhisiwi kufanya mabadiliko ya vipindi na kurusha matangazo mubashara bila kutoa taarifa TCRA na hatua za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa kwa kituo kitakachokiuka mwongozo huu.”

Kisaka alisema mwongozo huo mpya utaisaidia mamlaka hiyo kushughulikia malalamiko zikiwemo lugha chafu, au mtu kudhalilishwa wakati kipindi kinarushwa.

“Hii ni muhimu sisi kuwa na taarifa ya vituo hivi vinaporusha tukio mubashara kwa kuwa sasa kama sisi hatuna habari tunashindwa kulishughulikia lile tangazo,” alisisitiza.

Kisaka alisema pamoja na mwongozo huo hali za dharura zitapewa kipaumbele na mamlaka hiyo katika urushaji wa matangazo mubashara endapo taarifa za tukio zitachelewa kuwasilishwa nusu saa kabla.

Kuhusu vituo vya utangazaji vinavyochukua matangazo mubashara kutoka kwa wenzao, alisema pia ni lazima kutoa taarifa na kuingia makubaliano kabla ya kurusha matangazo hayo. “Usichukue kinyemela mtaarifu mkubaliane kurusha matangazo hayo,” alieleza.

Mtangazaji mwandamizi Hamza Kasongo alitoa angalizo kwa vituo hivyo katika eneo la taarifa ya habari kuwa makini kwa kuwa kipindi hicho ni muhimu kwa kituo chochote.

“Nimechagua somo hili kwa kuwa ndio nembo au roho ya chombo cha utangazaji. Ili watu wakuamini lazima uzingatie muda, maandalizi mazuri, uendeshaji wa taarifa mpaka hitimisho,” alisisitiza.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari aliahidi ushirikiano wa kutosha kwa vituo hivyo na kupanga vikao vya mara kwa mara ili kusikia mambo yanayoendelea na maeneo yanayohitaji maboresho zaidi na kuyafanyia kazi kama mamlaka.

“Najua kazi nzuri zinazoendelea mnazofanya, na kwamba kikao hiki ni sehemu ya kikao kazi kinachofanyika mara kwa mara,” alisema Dk Bakari.

Mwongozo uliotolewa Septemba 7, mwaka jana ulivitaka vituo hivyo vya utangazaji kutoa taarifa kwa TCRA wakati wa kurusha mubashara matukio ya sherehe za kitaifa ambazo ziko kwenye kalenda na matangazo mubashara ya dharura.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, matukio ya sherehe za kitaifa yalitakiwa kutolewa taarifa kwa mamlaka hiyo siku 14 kabla ya tukio wakati matukio ya dharura taarifa iwasilishwe kwa barua pepe kwa TCRA.

Chanzo: www.habarileo.co.tz