Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Teknolojia ya ukaushaji mazao  kujibu tatizo la sumu kuvu

Afa1c60cfac0b11ea4b3956846ac694b Teknolojia ya ukaushaji mazao  kujibu tatizo la sumu kuvu

Thu, 6 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UKAUSHAJI wa mazao kwa usahihi baada ya kuvunwa unaelezwa kuwa ni hatua muhimu kwenye kilimo chenye tija kwani kipimo kikubwa cha ubora wa mazao ni unyevunyevu uliopo wakati wa matumizi yake.

Mazao kama mahindi, maharage na mengineyo yanapaswa kukaushwa vizuri kwani yanapokuwa na unyevunyevu sahihi wakati wa kuhifadhiwa ghalani hupunguza uharibifu utokanao na wadudu au magonjwa na tatizo la sumu kuvu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Uyole kilichopo Mbeya, Dk Tulole Bucheyeki anasema mazao yanapokaushwa na kubaki na unyevunyevu sahihi, mbali ya kupunguza uwezekano wa mazao kupata sumu kuvu, huongeza uhakika na usalama wa chakula kwa walaji.

Dk Bucheyeki anasema hayo alipokuwa anakabidhi vifaa maalumu vyenye uwezo wa kukausha mazao mbalimbali hadi kubakia na unyevunyevu unaotakiwa.

Kwa mujibu wa Dk Bucheyeki, vifaa hivyo vimepatikana baada ya kufanyika utafiti wa pamoja kwa ushirikiano wa TARI na Bioversity International/ CIAT Alliance ukiwa na madhumuni ya kutumia vifaa hivyo kukaushia mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na maharage, mahindi na soya.

Katika kuleta tija zaidi na kipato kuongezeka, Bucheyeki anahimiza vifaa hivyo kutunzwa ili wakulima wengine wanaozunguka vijiji wavitumie na hivyo kunufaika na teknolojia hiyo rahisi yenye ufanisi mkubwa.

Mkurugenzi huyo anasema vifaa hivyo maalumu vya kukaushia mazao vilikabidhiwa kwa vikundi vya Upendo Senjele AMCOs cha Mbozi pamoja na kikundi cha Zinduka kilichopo Mshewe, Mbeya.

Naye mratibu wa shughuli za Bioversity International/ CIAT Alliance, Lazaro Tango anasema vifaa hivyo vinavyojulikana kama 'Solar Bubble Drier` vinaweza kukausha mazao ya aina mbalimbali.

Anasema mazao yanayoweza kukaushwa na vifaa hivyo ni maharage, mpunga, mahindi, soya, dengu, mbaazi, choroko, mtama, mbogamboga, matunda na kahawa.

“Vifaa hivi vinatakiwa kutumiwa vizuri kwani ufanisi wake hutegemea nishati ya jua, unyevunyevu kwenye hewa na unyevunyevu kwenye mazao,” anasema.

Kwa upande wake, mtalaamu wa tathmini na ufuatiliaji wa shughuli za Bioversity International/ CIAT Alliance, Sylivia Kalemera, anasema kukausha mazao kwa usahihi na haraka kutawapunguzia kazi akina mama na vijana.

Hali hiyo anasema itawawezesha wanawake na vijana kufanya kazi kwa urahisi, kwa muda mfupi na kubaki na muda wa ziada wa kufanya kazi zingine.

Mwenyekiti wa Upendo Senjele AMCOs, Daudi Bukuku anasema wakati wa kufanya biashara ya uhakika umefika kwa sababu soko la ndani na nje hutegemea mazao yenye ubora yaliyokaushwa vizuri na kufikia unyevunyevu unaokubalika.

Ofisa Kilimo Kata ya Nanyala anayefanyia shughuli zake katika kijiji cha Senjele, Shimba Ben Mwasaka anashukuru serikali ya Tanzania kupitia TARI Uyole na CIAT kwa kuleta vifaa vya kukaushia mazao ili kupunguza hasara kwa wakulima ambao mara kadhaa mazao yao hukosa soko kutokana kukosa viwango kutokana na ukaushaji duni.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Zinduka kilichopo kijiji cha Mshewe mkoani Mbeya, Witness Sikayanga anasema kutokana na kupata vifaa hivyo vya kukaushia mazao wamehamasika kujituma zaidi kwenye kilimo ili waweze kupata kipato kizuri.

Kwa maelezo yake kikundi kitazidi kufanya kazi kwa karibu zaidi na wanakijiji wengine ili nao wajifunze na kufaidika na teknolojia mbalimbali zinazotolewa na watalaamu wa kilimo.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, mtafiti mgunduzi na mbunifu wa mbegu mbalimbali za maharage, Dk Mary Ndimbo wa TARI Uyole anasema teknolojia hiyo itasaidia wakulima kupata mazao bora na salama na yenye upungufu wa sumu kuvu.

Dk Marry anasema njia mojawapo ya kupambana na sumu kuvu ni pamoja na kulima mbegu bora, kutunza vizuri mazao shambani na ghalani, kuvuna vizuri na kuyakausha vizuri ili kufikia unyevunyevu unaokubalika.

Naye Mtalaam wa Uchumi jamii wa TARI Uyole, Agnes Ndunguru, anasema teknolojia hiyo itaongeza watu watakaojihusisha na kilimo kwa sababu uwezekano wa kupata mazao yenye thamani kubwa na bora ni mkubwa sasa kwa kutumia vifaa hivyo maalumu vya kukaushia mazao.

Agnes anasema yamkini sasa soko la uhakika, mazao yanayofaa kwa kuchakata na bei nzuri itafikiwa baada ya kupatikana vifaa hivyo.

Kukausha vizuri na kwa haraka kunategemea kuongeza wanunuzi wa mazao, kuongezeka kwa soko, kuongezeka kwa tija na kupata lishe bora kwa kula chakula salama na hivyo kuongezeka kwa uhakika wa chakula kuanzia ngazi ya kaya na taifa.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo anasema teknolojia mbalimbali zilizogunduliwa na watafiti wa Kituo cha Uyole ni vema zikawafikia wakulima, kwani hazitakuwa na maana yoyote zisipotoa mchango kwa wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.

“Ili kilimo kiweze kuchangia uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla na ili mkulima aachane na kilimo cha kujikimu na kulima kibiashara, matumizi ya teknolojia (kama hiyo ya kukaushia mazao) ni muhimu,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tari, Dk Yohana Budeba amekuwa akiipongeza serikali kwa kuanzisha taasisi hiyo kwani imeleta mageuzi ya kilimo nchini kwa kujibu changamoto za wakulima kupitia tafiti mbalimbali zinazofanywa.

Anawashauri wakulima kutumia teknolojia ambazo zimeibuliwa na kutambuliwa na watafiti ili waweze kupata tija kwenye shughuli zao za kilimo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz