Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tawa yatakiwa kukusanya Sh100 bilioni kwa mwaka

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini(Tawa), imetakiwa kuongeza makusanyo yake kutoka Sh47 bilioni kwa mwaka hadi Sh100 bilioni ifikapo mwaka 2020.

Mwenyekiti bodi ya Tawa, Meja Jenerali mstaafu, Hamis Semfuko alitoa maagizo hayo jana Septemba 22, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maagizo ya bodi hiyo ambayo inamaliza muda wake.

Alisema lengo hilo linawezekana kwani Tawa tangu ilipoanza kazi rasmi mwaka 2006 imeweza kuwa na mafanikio makubwa baada ya kuanza fedha kidogo kiasi cha Sh 350 milioni pekee.

"Sasa tuna imani mamlaka imesimama na inaweza kutekeleza malengo, katika kipindi kifupi tumeweza kuwa na vitendea kazi ikiwemo magari 77" alisema

Mwenyekiti huyo pia aliwataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kuendelea kubadilika katika utendaji kazi wao, wawe wazalendo, waadilifu na kupiga vita rushwa.

"Tumewataka pia wajitahidi kuwa wabunifu kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii, watafute vitendea kazi vya kisasa zaidi na kuongeza michango kwa jamii inayozunguka mapori ya akiba," alisema.

Akizungumza baada ya maagizo hayo, mkurugenzi mkuu wa Tawa, Dk James Wakibara alisema mamlaka hiyo inaweza kufikia malengo ya kukusanya Sh100 bilioni kwa mwaka.

Dk Wakibara alisema kufikiwa lengo hilo kunawezekana kutokana na mikakati iliyopo ya mamlaka hiyo kuendelea kuboresha maeneo ambayo yanavutia watalii.

"Tunaboresha sekta ya uwindaji, utalii wa picha na tunajipanga kuwa na utalii wa uvuvi wa samaki aina ya tiger lakini tumeboresha mifumo ya makusanyo ya mapato yetu" alisema

Alisema kwa sasa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za uhifadhi na Serikali wameweza kudhibiti ujangili wa tembo.

"Katika eneo la Selous pekee kulikuwa kila mwaka ikipatikana mizoga ya tembo waliouawa 30 lakini sasa kwa miaka miwili tumeona mizoga mitano tu," alisema.

Alisema utulivu uliopo sasa sekta ya utalii umesababisha ongezeko la wanyama hasa tembo ambao wamekuwa wakitoka hadi maeneo ya nje ya hifadhi.

Dk Wakibara pia alieleza bodi iliyomaliza muda wake imetoa mchango mkubwa ambao umewezesha mamlaka hiyo kuwa imara na kutekeleza majukumu yake.

Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori inasimamia karibu eneo la asilimia 20 ya nchi ambalo limehifadhiwa likiwa na wanyamapori, vyanzo vya maji na vivutio vingine vya utalii kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz