Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tawa yaboresha maeneo ya utalii

Kili Elephant2 Tawa yaboresha maeneo ya utalii

Wed, 28 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), imeanza kuboresha miumdombinu katika maeneo ya utalii yakiwemo ya hifadhi ya urithi wa utamaduni wa dunia wa magofu ya Kilwa Kisiwani na Songomnara wilayani Kilwa, mkoani Lindi.

Akizungumza juzi katika uzinduzi wa hatua ya kwanza ya mradi wa uboreshaji miundombinu ya utalii pamoja na boti maalumu uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tawa, Hamisi Semfuko, alisema hatua hiyo inalenga kuvutia wawekezaji na huduma za utalii ili kuongeza mapato kwa mamlaka na serikali.

"Tawa ilifanya upembuzi na kubaini kuwa changamoto zinazokabili eneo hili ni pamoja na kukosekana kwa maliwato katika hifadhi, uchakavu wa gati la Kilwa Kisiwani, uhaba wa gati eneo la Songomnara na kukosekana kwa banda la mapokezi," alisema.

Kwa mujibu wa Semfuko, changamoto nyingine ni hoteli, maji safi na salama, maeneo ya kupumzikia wageni, vyombo vya usafiri wa baharini na nchi kavu na miundombinu mingine inayohitajika kuwekwa na kuboreshwa.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Tawa iliandaa mpango wa utekelezaji utakaogharimu Sh bilioni 2.1 ukitekelezwa kwa awamu tofauti kutegemea upatikanaji wa fedha.

Alisema awamu ya kwanza inatekelezwa kwa Sh milioni 246. Tayari asilimia 90 imekamilika na kugharimu Sh milioni 179.4.

Semfuko alisema kiasi hicho cha fedha kimetumika kuboresha miundombinu ya utalii ikiwemo gati la kupokea wageni, njia ya kutembelea vivutio na maliwato za kisasa.

Alisema matumizi mengine ni ununuzi wa boti ya kitalii yenye kioo kwa chini kuwezesha watalii kutembelea na kufurahia viumbe bahari katika eneo la hifadhi ya kihistoria la magofu ya Kilwa Kisiwani na Songomnara.

"Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa banda la mapokezi ya wageni na banda la kulaza wageni pamoja na ukarabati wa majengo ya kale ni pamoja na kujenga jengo la kuhifadhi vitu vya makumbusho," alisema.

Katika uzinduzi huo, Zambi aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Tawa kwa kuelekeza nguvu kuboresha miundombinu hiyo akisema hatua hiyo itakuza utalii Kusini mwa Tanzania.

Aliitaka Tawa ishirikiane na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuboresha miundombinu ya shule, huduma za maji safi na salama na zahanati kwa ajili ya kukidhi idadi kubwa ya wananchi Kilwa Kisiwani.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi, aliutaka uongozi wa mkoa, wilaya na vijiji vya Kilwa kushiriki kikamilifu kukuza uchumi wao kwa kutumia fursa zinazopatikana za utalii, badala ya kubaki kuwa ni watazamaji au washangiliaji.

Kijazi aliipongeza Tawa kwa kupiga hatua kubwa ndani ya mwaka mmoja tangu ilipoanza kusimamia eneo la hifadhi ya Kihistoria Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songomnara, hali iliyofanya watalii kuongezeka pamoja sambamba na ongezeko la mapato kutoka Sh milioni 12 hadi kufikia Sh milioni 40.

Chanzo: habarileo.co.tz