Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tatizo la mikopo kwa wafugaji wa samaki latafutiwa dawa

Wavuvi Mikopo Dawa.jpeg Tatizo la mikopo kwa wafugaji wa samaki latafutiwa dawa

Sat, 5 Nov 2022 Chanzo: Mwananchi

Serikali ikishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) imekutana taasisi za fedha kwa lengo la kuzijengea hamasa kuwawezesha wafugaji wa samaki ili kuongeza uzalishaji nchini.

Hatua hiyo ni kutokana na changamoto wanayopitia wafugaji wanapokwenda kukopa fedha kwa ajili ya ufugaji wa samaki, ambapo taasisi za fedha hukataa kutoa mikopo kwa kundi hilo kwa kudhani kuwa hazina faida.

Akizungumza katika kikao hicho leo Novemba 4, 2022 kilichohusisha wadau kutoka nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Mkurugenzi wa Ukuzaji wa viumbe maji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Nathael Madalla amesema, uwekezaji wa ufugaji samaki nchini na Afrika upo chini.

Amesema mwaka 2020 Afrika imezalisha tani milioni 2.3 ya samaki sawa na asilimia 1.9 ya uzalishaji ambapo Duniani tani milioni 122.6 ya samaki ilizalishwa.

"Benki zilikuwa zinaona ufugaji wa samaki kama biashara ya kupoteza na wakati huo huo wafugaji wanaona mabenki hawatoi mikopo, kwahiyo tumewaleta pamoja kuwajengea hali ya kuelewana.

“Tanzania tupo mbele kwa sababu benki zetu zimeanza kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki ambapo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) tayari imetoka Sh3.6 bilioni," amesema.

Dk Madalla amesema, ufugaji wa samaki umekuwa chanzo kikubwa cha chakula duniani ambapo kwa mwaka 2020 uzalishaji ulifikia tani milioni 122.6 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani milioni 87 ya wanyama wengine wa baharini.

"Kwa Tanzania uzalishaji umepanda kutoka tani 4,790 mwaka 2015 hadi tani 29,346.61 kufikia 2021 na Serikali imechukua jitihada kuhakikisha inakuza ufugaji wa samaki,"ameeleza.

Kwa upande wake Mwakilishi wa FAO nchini, Tipo Nyabenyi amesema, kupitia mkutano huo suluhu ya uwekezaji mdogo katika ufugaji wa samaki utapatikana hasa kwa kuendelea kuzijengea uelewa taasisi za kifedha fursa zinazopatikana katika mnyororo wa thamani wa ufugaji wa samaki.

Amesema fursa ambayo FAO inatoa kwa wafugaji wa samaki ni kuwapa ujuzi wa namna ya kuandika mpango wa biashara ambao utawawezesha kupata mikopo kwa urahisi.

Naye Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kilimo Benki ya NMB Wogofya Mfamalagoha amesema benki hiyo inatoa mikopo ya zana za uvuvi na ufugaji wa samaki.

Miongoni mwa zana alizotaja ni boti,nyavu za uvuvi na majokofu maalumu ya kuhifadhia samaki. Mfugaji wa Samaki wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Farida Buzohera amesema, mbali na changamoto ya mikopo kwa wafugaji wa samaki, hakuna viwanda vya kutengeneza chakula hatua inayowafanya kuagiza kutoka nje ya nchi.

Chanzo: Mwananchi