Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tari yawashauri wakulima wa korosho

D87753c266ee03f36049e8726590f1c9 Tari yawashauri wakulima wa korosho

Mon, 9 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) imewashauri wakulima wa korosho mikoa ya Kusini kuendelea kuhudumia mikorosho yao, kuokota korosho zinazokomaa na kuanguka hata baada ya msimu wa korosho kumalizika.

Kaimu Makurungezi wa Tari Naliendele, Dk Fortunus Kapinga ametoa ushauri huo kutokana na mikorosho katika baadhi ya maeneo kuanza kustawi na mauwa kuchipua upya, hali inayoashiria uwapo wa korosho zaidi hata baada ya msimu huu kumalizika.

Kapinga alisema maua ya korosho yameanza kuchipua upya kwa wingi kutokana na uwapo wa hali ya hewa nzuri ambayo imefanya mikorosho kustawi vizuri.

Alisema hali hiyo imejionesha zaidi katika maeneo ambayo awali yalikuwa na tatizo la kukauka kwa maua ya mikorosho kwa sababu ya baridi iliyotokana na kushuka kwa joto chini ya nyuzi joto 20 hadi kufikia 17 kuanzia Julai hadi Agosti mwaka huu.

Maua ambayo yalikauka kipindi cha baridi yalianza upya kuchipuka kati ya Septemba na Oktoba baada ya kurejea kwa hali ya hewa kati ya nyuzijoto 20 na 30 na kuruhusu kustawi kwa mikorosho.

“Hali hiyo huenda wakulima wakaiona sio ya kawaida na wengi wakaacha kuhudumia mikorosho yao na kuacha korosho nyingi shambani kwa kudhani msimu umeisha.”

“Wakulima wengi wamezoea kuacha kuokota korosho ifikapo Desemba kwa dhana kwamba msimu umeisha na kuongeza, tunawashauri waendelee kuhudumia mashamba yao kadiri maua yanapoendelea kuchipua na kutoa korosho.”

Alisema mikorosho hasa inayotokana na mbegu bora huwa ina kawaida ya kufidia uzao wa korosho ambazo hushindwa kukua vizuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kushuka au kupanda kwa nyuzi joto.

Katika msimu wa mwaka 2020/2021, Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ilitangaza matarajio ya kupata mavuno ya korosho tani 278,000 ilikinganishwa na mwaka juzi 2018/2019 ambapo ilikuwa ni tani 225,000 na mwaka jana 2019/2020 tani 232,000.

Chanzo: habarileo.co.tz