Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tari yaja na mbegu za kisasa kufufua zao la ulezi

Ulezi Zao Tari yaja na mbegu za kisasa kufufua zao la ulezi

Tue, 23 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KWA zaidi ya miaka 10 sasa mkulima kutoka Kata ya Mtiinko mkoani Singida, Juma Mene amekuwa akilima ulezi katika eneo lenye ukubwa wa ekari tano hadi 10. Mene anatumia mbegu za asili katika kilimo ambapo wastani wa mavuno kwa ekari moja ni gunia tano hadi sita.

Akizungumza na HabariLEO kuhusu utumiaji wa mbegu bora za kisasa, Mene anasema huwa hazipatikani katika maeneo yao na elimu kuzihusu ni ndogo kwao.

Anasema alifahamu kuwepo kwa mbegu bora za kisasa mwaka jana baada ya kuzungumza na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa mkoani Morogoro, lakini anakiri bado hajaanza kuzitumia. “Uhamasishaji wa kulima zao hili la ulezi umekuwa mdogo kwa kuwa wakulima wamekuwa wakilima kienyeji wakawa wanapata mavuno kidogo hivyo wakahamia kwenye alizeti.

“Miaka ya nyuma huku kwetu watu wengi walilima ulezi pia ni kutokana na uwepo wa soko, kwani soko kubwa lilikuwa Moshi sasa limeyumba,” anasema Mene. Akielezea mafanikio ya zao hilo pamoja na changamoto ya utumiaji wa mbegu za asili na kulima kienyeji, anasema ulezi soko lake halimtupi mkulima kama mazao mengine.

Mene anasema ukilima ulezi unaweza kuhifadhi hata miaka mitano bila kubanguliwa na japo soko lake limepungua wamekuwa wakiuza katika mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mwanza na nchini Kenya kwa kukusanya ulezi kutoka kwa wakulima na kuusafirisha kwa pamoja. Kwa maelezo yake kwa sasa bei iko chini kwani kilo moja ni Sh 1,200 lakini zamani waliuza kilo moja hadi Sh 2,500.

Anakiri changamoto iliyopo hadi bei kushuka ni kutokana na kutumia teknolojia duni ya kuuchambua ulezi huo kwani wakulima wamekuwa wakiupiga chini hivyo kuwa na mchanga mwingi kiasi kinachowafanya wakose soko. Anasema endapo itapatikana teknolojia ya kuukoboa itaongeza soko kwa kuwa hivi sasa wanunuzi wanakwepa kununua ulezi uliopigwa chini kutokana na kuwa na michanga mingi inakosa soko.

Mene anaeleza changamoto nyingine ni upatikanaji wa mbegu za kisasa kwani wakulima wengi hawazifahamu na jinsi ya kupanda kisasa. Pia anaeleza ukosefu wa mashine za kupandia ulezi ni changamoto kubwa, kuyumba kwa soko pamoja na ukosefu wa elimu kuhusu zao hilo kulimwa kisasa.

Kwa upande wake mzalishaji wa ulezi katika Kiwanda cha Nyirefami Ltd aliyeko mkoani Arusha ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu, Robert Nyirenda, anasema kiwanda hicho kinajishughulisha na usagishaji wa unga wa ulezi kwa malengo ya chakula. Anasema shughuli za kiwanda hicho zilianza mwaka 1992 na ulezi wananunua kwa wakulima wadogo vijijini. “Shida kubwa tunayokutana nayo ni maandalizi ya ulezi huo wakati wa uvunaji,” anasema Nyirenda.

Anakiri zao hilo halijapewa kipaumbele nchini wakati ulezi ni nafaka ambayo haiharibiwi kiurahisi na wadudu hivyo haihitaji unyunyiziaji wa dawa. Changamoto kubwa wanayokutana nayo ni wakulima kufanya udanganyifu katika soko la ulezi kwa kujaza mchanga, mawe, vyuma ili kuongeza uzito. “Uagizaji umekuwa changamoto kwetu kwa maana wengi wanaofanya shughuli hizi hawako rasmi,” anasema Nyirenda.

Kwani kuna wakati wanakosa ulezi kwa ajili ya uzalishaji hivyo kuagiza kutoka nje ya nchi hasa Zambia au Uganda kwa kuwa ni wazalishaji wazuri. Nyirenda anasema kiwanda chake kina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 10 kwa siku ila kutokana na changamoto ya mchanga unaokuwepo katika ulezi inabidi wazalishe chini ya kiwango hicho.

Kwa upande wake Mratibu wa Utafiti wa Mazao ya Mtama, Uwele na Ulezi Kitaifa, ambaye ni Mtafiti Mgunduzi wa Mbegu Tari Ilonga, Emmanuel Mwenda anasema kwenye zao la ulezi wana mbegu mpya tatu zimefanyiwa utafiti na zina matokeo tofauti na mbegu za asili. Anasema wanatafiti mbegu kuboresha zilizopo na kupata majibu ya changamoto za mkulima ikiwemo ya kuwa na kipato kidogo kwa sababu ya mbegu anazozitumia kutuchukua muda mrefu kukomaa ambayo ni miezi sita au saba.

Tari Ilonga imefanya utafiti ili kuwapatia wakulima mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi. “Mbegu ambazo tunazo ni U15 inafanya vizuri katika maeneo mengi isipokuwa kwenye maeneo ambayo ni baridi sana, mbegu hiyo inaathiriwa na ugonjwa wa fangasi lakini kuna mbegu inayojulikana kama P224 ina ukinzani wa kutosha dhidi ya ugonjwa huo.

“Mbegu ya U15 ilianza kutoka baada ya kuona upungufu huo katika eneo hilo la ugonjwa wa fangasi hasa katika maeneo yenye baridi, maeneo mengine inalimwa bila shida, tukasema tumpatie mkulima kilicho bora tukaleta mbegu inayojulikana kama P224 ikawa inaweza kudhibiti magonjwa ya fangasi vizuri,” anasema Mwenda.

Anasema mwaka 2021 imepatikana mbegu mpya inayojulikana kama TARIFM1 ambayo ina uzazi mkubwa kulinganisha na mbegu mbili za awali zilizokuwa zimetolewa. “Maana mbegu zile zilikuwa na uwezo wa kumpa mkulima mavuno mpaka kufikia tani mbili kwa eka moja ambayo ni takribani kama gunia nane kwa ekari.

Mbegu hii ya TARIFM1 ina mavuno kuanzia tani tatu mpaka nne mkulima akifanya vizuri utaweza kuona kwamba ni kiwango kikubwa sana cha tija kwa maana ya gunia kuanzia 10 mpaka 20 kwa ekari,” anasema. Anasema faida ya zao hili ni pamoja na kustahimili ukame kwani kundi la mazao ya mtama, uwele na ulezi hustahimili ukame ni mazao ambayo yanaweza kumsaidia mkulima kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa sehemu nyingi hazipati mvua za kutosha.

“Lakini ulezi una madini ya calcium mengi zaidi kuliko nafaka yoyote unayoijua duniani, kwa maana ya kwamba kiwango kilichoko kwenye ulezi ni karibu mara 10 ya calcium iliyoko kwenye ngano ambayo haijakobolewa. Lakini ina virutubisho vingi zaidi karibu hata mara 20 ambavyo vipo kwenye mahindi au viko kwenye mpunga,” anasema. Anasema watoto wengi ambao unawakuta wana matege ni kwa sababu ya ukosefu wa madini ya calcium.

“Lakini madini yaliyopo ya calcium kwenye ulezi ni zaidi ya mara mbili ya madini haya yanayopatikana kwenye maziwa ya mama hivyo utagundua ni muhimu sana kwenye lishe ya mtoto,” anasema. Anasema nafaka hiyo pia hutumika kwa staili tofauti, wako wanaotumia kama chakula kwa ajili ya uji lakini pia katika mikoa ya Kusini wazee wamekuwa wakila ugali wa ulezi. Kuhusu soko la nafaka hiyo anasema halijawahi kuyumba ni kubwa na hasa ikilinganishwa kwamba uzalishaji wa ulezi unazidi kupungua mwaka hadi mwaka kwa sababu ya mazao mengine ambayo yameingia.

Anasema kwa sasa tani 80,000 zinalimwa na hekta 80,000 zinatumika. Anataja mikoa inayolima ulezi kwa wingi kuwa ni Kanda ya Kati Dodoma na Singida, Kanda ya Ziwa ni Shinyanga, Mara, mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni Mbeya, Njombe, Katavi na Rukwa.

Anashauri wakulima kulima ulezi kwa wingi ili kupunguza magonjwa, lakini pia kuwa na soko la uhakika. Kuhusu teknolojia bora ya zao hilo anasema kazi ya kupeleka teknolojia kwa wakulima si ya mtu mmoja ni ya kuitaji muunganiko wa wadau wengi, maofisa ugani na wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali. Anakiri kuwa wakulima wengi bado hawajui mbegu bora ni zipi, kanuni bora ni zipi, bado hawapati masoko ya kutosha pamoja na kwamba masoko yapo lakini taarifa za masoko haziwafikii kwa wakati hivyo kwa umoja taarifa zinaweza kuwafikia wengi. Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inakadiriwa kuwa mahitaji ni zaidi ya tani 200,000 kwa mwaka. Na kwamba kwa msimu wa mwaka 2019/20 zililimwa hekta 31,468 za ulezi ambapo tani 32,959 zilizalishwa. Na mikoa inayoongoza kwa uzalishaji ni Rukwa tani 8,853, Dodoma tani 5,420 na Singida tani 4,423.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live