Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tari Kihiga wazalisha mbegu bora za chikichi  4,205,335

57567f388ed0df6401e0176f22b8e49e Tari Kihiga wazalisha mbegu bora za chikichi  4,205,335

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imefanikiwa kuzalisha mbegu bora milioni nne za zao la chikichi kama sehemu ya mkakati wa kutaka kuokoa fedha za Serikali zaidi ya shilingi bilioni 443 ambazo zimekuwa zikitumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya wakati wa kutembelea, kukagua na kujionea shughuli za maendeleo ya Sekta ya Kilimo mkoani Kigoma Kituo mahiri cha utafiti wa zao la chikichi (TARI Kihinga) katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji.

Aidha katibu Mkuu huyo alisema kwamba Wizara ya Kilimo imefanikiwa kuimarisha shughuli za utafiti wa zao la michikichi kwa kukipatia kituo utafiti cha TARI Kihinga Shilingi Bilioni 1.4 kuzalisha miche ya michikichi na ununuzi wa vitendea kazi vya watafiti.

Kusaya alibainisha kuwa tangu kituo cha utafiti wa zao la michikichi kianzishwe mwaka 2019 kufikia Desemba 10, 2020 kituo cha TARI Kihinga kimezalisha zaidi ya mbegu bora 4,205,335 za zao la chikichi na zimetolewa kwa Halmashauri sita za mkoa wa Kigoma; zinazolima zao hilo.

Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Kigoma – Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Mji wa Kasulu, Wilaya ya Uvinza na Wilaya ya Buhigwe.

Kusaya alisema mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 570,000 kila mwaka ambapo uwezo wa nchi kuzalisha ni tani 205,000 sawa na asilimia 36 na kuongeza kuwa kiasi cha tani 365,000 sawa na asilimia 64 ya mafuta huagizwa toka nje na kuigharimu nchi kiasi cha shilingi biloni 443 kila mwaka.

“Huwezi kukabiliana na changamoto ya namna hiyo bila ya kuanza na mbegu, ndiyo maana tumeona tuanze na mbegu bora kwanza, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alitoa maelekezo ya kuondokana na utegemezi huo 28 Julai, 2018 baada ya kufanya kikao na Wadau ili kuweka mkakati wa upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kupitia uendelezaji wa zao la chikichi,”alisema.

Kusaya aliongeza kuwa serikali imeamua kuanza na mkoa wa Kigoma na kuongeza kuwa zaidi ya mikoa 16 imeonyesha kuwa na fursa ya kupanda zao la chikichi.

Katika Taarifa yake kwa Katibu Mkuu Kilimo, Gerald Kusaya Msimamizi wa Kituo cha TARI Kihinga Dk Filson Kagimbo alisema hadi sasa kiasi cha mbegu 1,863,111 zilishatolewa kwa taasisi za umma na sekta binafsi.

Alizitaja taasisi hizo ni pamoja na TARI Kihinga yenyewe (120,000), JKT Bulombora (219,691), Gereza la Kwitanga (286,125), Gereza la Ilagala (15,795), Shamba la Wakala wa Mbegu za Kilimo, ASA - Bugaga (50,000), Taasisi ya Utafiti Ilonga – TARI Ilonga (235,500) na Sekta Binafsi mbegu (936,000). Baada ya Taasisi hizo kupewa mbegu hizo ambapo jumla ya miche 1,087,143 imezalishwa.

Dk Kagimbo aliongeza kuwa halmashauri sita za mkoa wa Kigoma zilipewa miche 306,000 ambapo jumla ya miche 183,175 ilizalishwa. Halmashauri hizo ni pamoja na Manispaa ya Kigoma – Ujiji, Wilaya ya Kigoma, Wilaya ya Kasulu, Mji wa Kasulu, Wilaya ya Uvinza na Wilaya ya Buhigwe.

Wakati huo huo katibu Mkuu, Kusaya amekabidhi trekta kama sehemu ya kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mbegu bora pamoja na miche kwa kituo cha TARI Kihinga.

Trekta hilo lenye thamani ya shilingi milioni 75 limekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Taasisi hiyo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Chanzo: habarileo.co.tz