Dar es Salaam. Katika jitihada za kusikiliza kero, Serikali imekutana na wawekezaji wa Kimarekani waliopo nchini kujadili namna ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kampuni 47 kati ya 238 za Kimarekani zilizopo nchini, Kaimu Balozi wa Marekeni, Dk Inmi Patterson amesema umefika wakati wa Tanzania kuacha maneno na kusimamia mipango yake ili kujieletea maendeleo.
“Sekta binafsi iaminike na ipewe fursa kubwa zaidi kuchangia kujenga uchumi imara,” amesema Balozi Inmi.
Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje pamoja na Angellah Kairuki anayesimamia uwekezaji ni mawaziri wanaozungumza na wawekezaji hao na kutafuta suluhu ya kero walizonazo.
"Tunachukua hatua nyingi kuboresha mazingira. Tumeshaanza kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini," amesema Kairuki.
Kwa upande wake, Profesa Kabudi amesema zamani ni wafanyabiashara wa nje walikuwa wanasikilizwa lakini sasa hata wa ndani wanapewa kipaumbele.