Bariadi. Serikali ya Tanzania imezindua mifumo mitatu yatakayotumika kuendeleza, kuboresha na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Mifumo hiyo imezinduliwa jana Alhamisi Agosti 8, 2019 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa katika viwanja vya Nyakabindi wikayani Bariadi mkoani Simiyu wakati wa kilele cha maonesho ya Nanenane kitaifa.
Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga alitaja mfumo wa kwanza ni ule wa masoko inayoweka uwazi na kuunganisha wakulima na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.
"Mfumo wa pili ni wa usimamizi wa biashara ya sekta ya kilimo kwa njia ya kielektroniki," alisema Hasunga
Waziri Hasunga alitaja mfumo wa tatu ni wa usajili na kanzi data ya wakulima inayoonyesha idadi yao, aina ya mazao wanayolima, ekari wanazolima na matarajio ya mavuno yao kila msimu.
Akizindua mifumo hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza michakato yote yanayohusu maendeleo ya sekta ya kilimo kushirikisha wadau wote kuanzia wakulima kupitia vyama vyao vya msingi (Amcos), taasisi za fedha, wataalam, taasisi za kilimo na viongozi kuanzia ngazi ya msingi.
Pia Soma
- Sakata la kampuni iliyofutiwa umiliki wa kitalu Arusha lachukua sura mpya
- Kimenuka Afrika Kusini, Polisi yakamata raia 600 wa kigeni
- Nyakabindi kuwa kituo cha kudumu mafunzo ya kilimo
Kiongozi huyo aliziagiza mabenki na taasisi zote za kifedha kuhakikisha huduma zao zinawafikia wakulima vijijini.
"Mabenki yafungue matawi au kuweka mawakala hadi vijijini kuwezesha wakulima kufungua akaunti na kupata huduma za kibenki ili kuongeza usalama wao na fedha zao wakati na baada ya mavuno," alisema
Alitoa mfano wa tukio la kukuta boksi iliyojaa mamilioni ya fedha katika jengo la mabati ya moja ya chama cha msingi cha ushirika wilayani Bariadi walikokuwa wanalipwa wakulima wa zao pamba.
"Viongozi wale wa Amcos watafanya kazi ile ya malipo karibia kutwa nzima na fedha zikibaki zilale kwenye lile jengo la bati. Wakulima wale wangekuwa na akaunti wangelipwa kwa njia ya benki; siyo tu ingewaondolea usumbufu wa kupanga foleni kutwa nzima, bali pia ingewahakikishia usalama wao binafsi na fedha zao," aliongeza
Waziri Mkuu Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na wenzake wa mikoa mingine inayolima pamba kuhakikisha ulinzi wa kutosha wakati wote wa ununuzi na malipo ya wakulima kupitia Amcos zao.