Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yavutiwa na faida mkataba wa Irena

Dkt Biteko: Watanzania Wanahitaji Mafuta Kwa Urahisi Tanzania yavutiwa na faida mkataba wa Irena

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Tanzania ikijiunga na Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (IRENA) itanufaika na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu na pia itanufaika na programu za nchi za kusini na Mashariki mwa Afrika kwa ajili ya mifumo unganishi ya kusafirisha umeme.

Dk Biteko ameyasema hayo leo, jijini Dodoma wakati akifunga Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ililenga kuwapa uelewa Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu Mkataba wa IRENA ambapo Tanzania imeonesha nia kujiunga na mkataba huo kutokana na faida zake.

“Faida nyingine ambazo Tanzania itapata ikijiunga na Mkataba wa IRENA ni kunufaika na mikopo mbalimbali ya kufanya tafiti, kuibua na kuendeleza miradi ya Nishati Jadidifu inayotolewa kwa nchi wanachama na kupata misaada ya kiteknolojia kwa ajili ya uendelezaji wa nishati Jadidifu,” amesema Biteko

Amesema, Tanzania pia itanufaika na ufadhili wa mafunzo ya Nishati Jadidifu kwa kuwajengea uwezo watalaamu wa kitanzania katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya Nishati Jadidifu pamoja na kunufaika na tafiti za kiteknolojia za nishati jadidifu kupitia vyuo vya hapa nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mathayo David amesema kuwa, kamati yake inaunga mkono Tanzania kuingia katika mkataba huo wa IRENA ili kuweza kunufaika na fursa zilizopo.

IRENA ni Taasisi iliyoanzishwa mnamo Januari, mwaka 2009 na ilianza kutekeleza majukumu yake mwezi Aprili 2011 ambapo Tanzania ipo katika taratibu za kujiunga na Taasisi hiyo. -

Chanzo: www.tanzaniaweb.live