SOKO la kahawa limeendelea kuwa zuri duniani na hadi wiki ya kwanza ya Januari mwaka huu, tani 54, 000 zilikuwa zimepata soko la nje na hivyo kuliingizia taifa Dola za Marekani zaidi ya milioni 111 (bilioni 257.4/-).
Kwa mujibu wa taarifa za mwenendo wa masoko, zilizotolewa na Wizara ya Kilimo, sehemu ya masoko ya mazao ya kilimo hadi kufikia Januari 8 mwaka huu kahawa yote iliyoingia sokoni katika msimu wa mauzo wa 2020/21, ilipata soko la nje.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa masoko ya aina tatu ya zao hilo yalifanywa ambapo jumla ya kilo 19,314,171 za kahawa aina tatu ziliuzwa kwenye mnada na kuingiza Dola za Marekani milioni 50,743,357.
Aina hizo ni arabika laini iliyouzwa kilo 17,833,803 kwa mnada na kupata thamani ya Dola za Marekani milioni 48,300,950, kahawa ya arabika ngumu iliuzwa kilo 123,178 iliyoingiza Dola za Marekani 228,689 na kahawa aina ya robusta iliuzwa kwenye mnada jumla ya kilo 1,357,190 na kuingiza pato la Dola za Marekani milioni 2,213,719.
Katika soko la moja kwa moja katika msimu wa mauzo mwaka 2020/21, Kahawa aina ya arabika laini ya jumla ya kilo milioni 8,140,831 ziliuzwa na kuingiza pato la Dola za Marekani milioni 25,379, 522 huku kahawa ya arabika ngumu kilo 1,144,860 iliuzwa na kuingiza Dola za Marekani milioni 2,118,550.
Aidha, kahawa ya robusta yenye kilo 25,364,700 iliuzwa kwenye soko la moja kwa moja nje ya nchi na kuingiza pato la Dola za Marekani milioni 32,595,975.
Kuhusu kahawa iliyouzwa viwanda vya ndani, taarifa hiyo ilisema jumla ya kilo 152,217 za kahawa aina ya arabika laini na robusta iliuzwa na kuingiza pato la Dola za Marekani 177,812.
Julai mwaka jana, Mkurugenzi wa Ubora na Masoko wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimario, alisema bei ya kahawa imepanda na kuwafanya wakulima wa zao hilo kufurahia ambapo kwa msimu wa mwaka 2019/20 jumla ya tani 59,318 zilipata soko la nje na kuingiza pato la Dola za Marekani Milioni 112.8
Kimario alisema kahawa hiyo imeuzwa kwenye masoko katika nchi za Marekani,China,Japan na hivi karibuni wamepata masoko kwenye nchi za Falme za Kiarabu (UAE).
Wakati hali ya bei ikiwa hivyo, wizara imeendelea kusisitiza na kuwataka wenye maduka ya pembejeo na wafanyabiashara za zana za kilimo kuhakikisha wanauza mbolea kwa bei elekezi iliyotangazwa Novemba 30 mwaka jana kwa kuzingatia mkoa na aina ya mbolea.
Katika bei hiyo elekezi, mbolea aina ya DAP, ya mfuko wa kilo 50 bei elekezi ni kati ya shilingi 60,973 hadi shilingi 70,957 kulingana na mkoa, mkulima yuko na ile ya kilo 25 bei elekezi ni kati ya Sh 31,486 hadi Sh 36,478.
Aidha, mbolea aina ya Urea kwa mfuko wa kilo 50 bei elekezi iliyopangwa na wizara ni kati ya Sh 47,791 hadi Sh 57,395 kulingana na mkoa husika na ile ya kilo 25 bei ni kati ya Sh 24,896 hadi Sh 29,697.
Hata hivyo, wizara hiyo imetoa ratiba kwa baadhi ya mazao ya viungo na matunda (hot culture) kwa wakulima ya kuwasaidia kulima,kuvuna na kupata bei nzuri ambayo inaonesha kuwa kwa wakulima wa vitunguu na nyanya muda sahihi wa kupanda ni kuanzia Septemba hadi Desemba.
Kadhalika, kwa wakulima wa matango na viazi mviringo msimu sahihi wa kupanda ni Desemba hadi Februari, huku wakulima wa tangawizi wakiaswa kupanda zao hilo kuanzia Desemba hadi Februari na wakulima wa karoti wakiaswa kupanda kuanzia Julai hadi Oktoba.