Wakati Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) likiendelea, Tanzania imesaini mikataba ya kuendeleza kilimo ya zaidi ya Sh1 trilioni huku ikiendelea na mazungumzo na wadau wengine likiwamo Shirika la Maendeleo ya Kilimo la Umoja wa Afrika (IFAD).
Mikataba hiyo imesainiwa kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na nchi ya Norway.
Hayo yalielezwa juzi jioni na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa na kuongeza kuwa, mkutano huo umekuwa na mafanikio kuliko matarajio yaliyokuwapo awali.
“Nchi inapoandaa mikutano hii inakuwa na malengo yake na sisi lengo letu lilikuwa ni kupata fedha kwa ajili ya kilimo. Juzi tumezindua programu ya P for R (mradi wa umwagiliaji) ya Dola 300 milioni za Marekani (Sh751.5 bilioni) ya Benki ya Dunia. Pia tunamalizia mazungumzo ya mkataba na Benki ya Maendeleo ya Afrika Dola 100 milioni (Sh250.5 bilioni),” alisema Bashe.
Alisema pia, wamesaini makubaliano (MoU) na Norway kwa ajili ya ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) kwa ajili ya kuboresha utafiti.
“Vilevile nilikuwa na maongezi na waziri mdogo wa kilimo wa Marekani na tumefikia mwafaka wa kuendeleza mradi wa Feed the Future na kushirikiana katika maendeleo ya matunda na mbogamboga,” alisema Bashe.
Mbali na makubaliano hayo, alisema wanaendelea na mazungumzo na IFAD ambao awali waliahidi kutoa Dola 60 milioni za Marekani (Sh150.3 bilioni).
“Bado tunaendelea na mazungumzo. Jana (juzi) Makamu wa Rais alikutana na Rais wa IFAD Ikulu ya Dar es Salaam na mimi nimekutana a uongozi wa IFAD kwa ajili ya kujadiliana hilo jambo,” alisema.
Pia, alisema katika jukwaa hilo, Serikali imezindua ofisi ya Maboresho ya Kilimo (Agricultura transformational office).
“Kama nchi tunajiandaa kuandaa mpango wa mwaka 2050 ambao ni lazima uendane na mpango wa kilimo,” alisema Bashe.
Pia, alisema wanaendelea na mazungumzo na Shirika la Misaada la Japan (Jica) kwa lengo hilo hilo la kupata fedha za kilimo.
Alisema kutokana na mazungumzo yote hayo, wanakusudia kuanzisha utaratibu wa kuweka misaada yote ndani ya kapu moja ili iwe rahisi kuifuatilia.
“Kumekuwa na tatizo la wafadhili kila mmoja anafanya kitu chake kidogo, sasa tumesema tunahitaji kufanya pamoja yaani kukusanya fedha zote kwenye kapu moja, kwa hiyo bado mazungumzo yanaendelea,” alisema Bashe.
Akifafanua kauli yake ya kutaka nchi za Afrika ziinuane badala ya kushindana, alisema kilimo kinahitaji fedha na kila nchi ina mambo yake ya kushindania.
“Biashara ndani ya Afrika haizidi asilimia 17, yaani sisi kwa sisi hatufanyi biashara kwa sababu tumeshindwa kutambua uwezo wa kila nchi kuzalisha bidhaa fulani,” alisema.
CPB yatafuta wabia
Katika mkutano wa AGRF unaoendelea, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) imeweka wazi maeneo matano inayotafuta wabia ili iweze kupanua wigo wake wa ufanyaji kazi.
Baadhi ya maeneo hayo ni lile la upatikanaji wa fedha kwa ajili uendelezaji shughuli zao, teknolojia, usambazaji wa bidhaa za wakulima wakubwa na wadogo pamoja na ukusanyaji wa mazao.
Mwenyekiti wa CPB, Salum Awadh Hagan, alisema bodi hiyo inahitaji wabia tofauti ili iweze kujiendesha kibiashara na kuwahakikishia wakulima soko la mazao yao katika maeneo wanayofanyia kazi.
Hagan alisema hayo wakati akizungumza na washiriki mbalimbali wa mkutano huo wa AGRF uliolenga kutangaza fursa zinazopatikana ndani ya bodi hiyo.
“Tunatafuta wabia wenye mitaji ya fedha, teknolojia, usambazaji wa bidhaa na wakulima wakubwa ili kufikia malengo yetu kama bodi, pia tunataka kutoka katika uuzaji wa rejareja na kuhamia katika uuzaji wa bidhaa kwa jumla,” alisema Hagan.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CPB, Gungu Mibavu alisema ili kufikia malengo yao pia wanahitaji mawakala wa kusambaza na kuuza bidhaa zao nchini, kukusanya mazao kutoka kwa wakulima kwa kile alichokieleza kuwa waliopo hawatoshi.
“Mazao tunayoshughulika nayo kwa sasa ni mahindi, mpunga, ngano, alizeti pamoja na mbaazi,” alisema Mibavu.
Wakati akisema hayo pia alielezea kuwa tayari bodi ina mikataba ya kibiashara ya kuuza mazao katika nchi za Rwanda na Burundi, wanayonunua kwa wakulima nchini.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema bodi hiyo inakusudia kutafsiri kwa vitendo malengo ya jukwaa hilo kwa kujumuisha vijana na wanawake katika uzalishaji wa mazao ya chakula.
“Bodi imejiandaa kukuza sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko ambayo ni muhimu katika mifumo ya chakula na kuchangia kapu la chakula la taifa,” alisema Silinde.
Pia, alisema mkutano huo unalenga kuchochea ushirikiano wa kibiashara na kampuni zinazoagiza nafaka kutoka Tanzania ili kuwa na mifumo endelevu ya chakula jambo litakaloongeza fursa na kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo.