Benki ya Dunia imeidhinisha mkopo wa Sh trilioni 1.8 (dola milioni 775) kwa ajili ya kuboresha uchumi na huduma za afya.
Shirika la Kimataifa la Maendeleo (IDA) lililo chini ya Benki ya Dunia limeidhinisha mkopo wa Sh trilioni 1.1 (dola milioni 500) kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya uchumi na mkopo wa Sh bilioni 581 (dola milioni 250) na msaada wa Sh bilioni 58.1 (dola milioni 25) kwa ajili ya programu ya Afya ya Mama na Mtoto.
Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa jana imeeleza kuwa mkopo huo utaisaidia Tanzania kutokana na kuyumba kwa sekta ya utalii na kukumbana na kupanda kwa bidhaa inazoagiza nje kama petroli na bidhaa nyingine kulikosababishwa na janga la Covid-19 na vita baina ya Ukraine na Urusi.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Nadhan Belete alisema: “Benki ya Dunia inasaidia sera zenye kuinua sekta binafsi ili kusaidia nchi kuboresha uchumi wake.”
Sehemu ya pili ya mkopo huo wa dola za Marekani milioni 275 utaisaidia nchi kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Hiyo ilielezwa kwamba inahusisha dola za Marekani milioni 250 kwa ajili ya Programu ya Kupima Matokeo (PforR) kwa Tanzania Bara na dola za Marekani milioni 25 kwa Mradi wa Uwekezaji Kiuchumi (IPF) kwa Zanzibar.
Mradi huo umeongezewa msaada wa dola milioni 25 kutoka Mfuko wa Dunia wa kusaidia wanawake, watoto na vijana.
Wanufaika wa programu hizo ni wanawake wenye uwezo wa kuzaa, vijana na watoto wa chini ya miaka mitano ikiwemo wachanga ambao ni asilimia 40 ya watu wote. Hao watasaidiwa huduma za afya na lishe.
“Kwa miongo miwili Tanzania imefanikiwa kupunguza magonjwa na kuboresha huduma za afya kutokana na kuboresha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na utoaji wa chanjo wa magonjwa mbalimbali,” alisema Mkurugenzi Mkazi wa Mipango na operesheni, Amit Dar na kuongeza:
“Kwa fedha hizi tunategemea kupata maendeleo mazuri kwenye maeneo ya kupunguza vifo vya akinamama, kupunguza vifo vya watoto wachanga na wenye utapiamlo.”