Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yapata ajira 10 EAC

D796ec1ebf24d5224b6bf275dc7deba0.jpeg Tanzania yapata ajira 10 EAC

Tue, 28 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania imepata nafasi 10 za ajira kati ya 37 katika mchakato wa ajira wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika kuanzia mwezi Oktoba 2021 hadi Aprili 2022.

Nafasi hizo ziliwaniwa na waombaji 15,000 kutoka nchi sita za jumuiya hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula alisema ajira hizo zilitangazwa kwa nchi sita wanachama wa EAC ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Burundi na Rwanda.

Kwa sasa EAC ina mwanachama mpya ambaye ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Alisema wizara inaendelea kuratibu fursa za ajira katika jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa. Mchakato huo wa ajira uligubikwa na sintofahamu baada ya kutangazwa na kulazimika kuingiliwa kati na Baraza la Mawaziri wa EAC na kuurejesha upya Januari mwaka huu kwa walioitwa kufanya usaili kupangiwa upya kuanza kufanya usaili.

Taarifa ya Sekretarieti ya EAC kwa umma iliyolifikia HabariLEO Afrika Mashariki, ilisema nafasi hizo zilitangazwa kujaza nafasi zilizokuwa wazi na waombaji 15,000 kutoka nchi zote za Jumuiya waliomba na waliokidhi waliitwa kwa ajili ya usaili. Lakini baadaye mchakato huo uliingia dosari kwa kupingwa na baadhi ya nchi baada ya kutolewa kwa majina ya walioitwa kwa ajili ya usaili na kulazimika mchakato huo kusitishwa kwa muda.

Baadaye, Baraza la Mawaziri la EAC lilitangaza kuendelea kwa mchakato wa kuajiri nafasi zilizositishwa Oktoba mwaka jana huku wakitaka baadhi ya nafasi za ajira kutangazwa upya. Baraza la mawaziri liliitaka sekretarieti kutangaza upya nafasi ambazo waliitwa kwenye usaili walitoka nchi moja mwanachama pamoja na kutangaza upya nafasi ambayo mtu mmoja pekee ndie aliitwa kwenye usaili.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Mawaziri wa EAC na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya, Adan Mohamed, alisema baraza katika majadiliano yake lilibaini kuwa mchakato wa kuajiri ulikuwa na kasoro. Alisema ili kuhakikisha usawa kati ya nchi wanachama katika mchakato wa kuajiri, mwenyekiti wa kamati alisema nafasi 11 kati ya zilizokuwa wazi zitatengwa kwa ajili ya Sudan Kusini.

Hii ni kwa mujibu wa agizo la Baraza namba 41 kwa Sekretarieti kuhakikisha Sudan Kusini inapata nafasi 11 kati ya 15 ambazo bado hazijaorodheshwa katika mchakato wa kuajiri EAC. Baraza la Mawaziri liliiagiza Sekretarieti kutangaza tena nafasi tatu za Uganda, ambazo ni mhariri wa hansard; mwandishi wa hansard na karani msaidizi mwandamizi. Kikao hicho kilibaini kuwa kulikuwa na makosa katika matangazo ya nafasi tatu zilizowaondoa wagombea kutoka Uganda na kupendekeza Sekretarieti kutangaza upya nafasi hizo.

Mawaziri walibaini kuwa kwa nafasi ambazo ni wagombea kutoka nchi moja, washirika pekee ndio wameorodheshwa, zilitakiwa kupitiwa upya ili kuhakikisha inatoa fursa ya ushindani. Mkutano huo pia ulibainisha kuwa baadhi ya matangazo yalikuwa na vikwazo vingi na yalihitaji uhakiki ili kuwezesha waombaji wengi kutuma maombi ya kazi hizo. Mkutano huo ulibainisha kuwa si halali kwa nafasi kupata mgombea mmoja pekee anayekidhi matakwa.

Mawaziri waliiagiza sekretarieti kuendelea na kazi za kuajiri nafasi zote ambazo hazikutolewa maagizo kuanzia Januari 2022 na kusisitiza kuwa, Burundi itapewa kipaumbele katika uajiri wa awamu ijayo ya kuajiri kwa mujibu wa maagizo ya Kikao cha 39 cha Baraza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live