Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yakabidhi rasmi msaada Malawi

STegomena Malawiiiii (600 X 346) Tanzania yakabidhi rasmi msaada Malawi

Tue, 21 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax kwa niaba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekabidhi rasmi msaada wa kibinadamu kwa Serikali ya Malawi kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa kimbunga Freddy kilichosababisha mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo Machi 13, 2023 na kusababisha madhara mbalimbali, ikiwemo vifo vya zaidi ya watu 400.

Msaada huo umekabidhiwa kwa Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera, jana Machi 20, 2023 katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Lilongwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Malawi na Tanzania, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Nancy Tembo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Humphrey Polepole.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Dk Tax amesema Rais Samia ametoa msaada wa kibinadamu na salamu za pole kwa Rais wa Malawi, Dk Chakwera pamoja na wananchi wa nchi hiyo kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo ikiwemo vifo, majeruhi, ukosefu wa makazi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ikiwemo barabara.

Msaada wa kibinadamu uliotolewa ni fedha taslimu na vifaa mbalimbali wenye ya thamani ya Dola za Marekani Milioni Moja. Msaada huo pia unajumuisha chakula, vifaa vya kuokolea, vifaa vya kujihifadhi, helikopta 2 za kijeshi zitakazotumika kupeleka misaada katika uokoaji pamoja na wanajeshi 100 watakaoshiriki kusambaza msaada huo, mahema 50; blanketi 6,000; tani 1,000 za unga wa mahindi na fedha taslimu kiasi cha Dola za Marekani 300,000.

Kwa upande wake, Rais wa Malawi, Dk Chakwera amemshukuru Rais na wananchi wa Tanzania kwa msaada uliotolewa kwao na kueleza furaha yake kwamba msaada huo umewafikia kwa haraka na kwa wakati na kwamba hii si mara ya kwanza Tanzania kuisaidia Malawi, kwani iliwahi kufanya hivyo mwaka 2015, mwaka 2019 na mwaka huu 2023.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live