Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yachangamkia soko la soya China

4fa992bad99aed1a407cdfe1243cdf01.png Tanzania yachangamkia soko la soya China

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imeanza kuchangamkia soko la maharage ya soya nchini China ambapo Machi mwaka huu imepeleka tani 140.

Sambamba na hilo imeruhusu wafanyabiashara Watanzania wa nchini kununua maharage hayo nje ya nchi na kuyapeleka kwenye soko hilo la China.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alieleza hatua hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge Humphrey Polepole (CCM) aliyetaka kufahamu mkakati wa serikali wa kukidhi soko la maharage ya soya kutoka China.

Katika swali lake, Polepole alisema: "China inatumia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 40 kwa mwaka kununua maharage ya soya kutoka nchi 12 duniani na Tanzania hivi karibuni tumesaini mkataba nao na kuwa nchi ya 12 kupata soko hilo.”

"Tunatakiwa kupeleka kwa mwaka tani laki 400 na sisi uzalishaji wetu ni tani 14,000 kwa mwaka hivyo serikali imejipangaje kutumia soko la China wakati uzalishaji wetu ni mdogo?"

Akijibu, Bashe alisema serikali imeshaipa kazi Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kuongeza uzalishaji wa mbegu pamoja na kuondoa ukiritimba kwenye kusajili wafanyabiashara.

"Tumeruhusu wafanyabiashara Watanzania mwaka huu kuagiza nje maharage ya soya na kupeleka China huku tukihakikisha uzalishaji nchini unaongezeka," alisema.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani, (Chadema), aliitaka serikali kubadili utaratibu wa kukopesha wakulima matrekta kutokana na mfumo uliopo unawasababishia hasara. Mbunge huyo alisema utaratibu unaotumika hivi sasa unawasababishia hasara kwa kuwa wanatozwa riba kubwa.

"Je, kwa nini serikali isibadili utaratibu unaotumika sasa kuwakopesha wakulima matrekta ili kuleta tija?" alihoji.

Akijibu swali hilo, Bashe alisema mikopo ya pembejeo na zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa wakulima hutolewa kupitia mifumo mbalimbali.

"Mojawapo ya mifumo hiyo ni kupitia sekta binafsi ambapo kampuni zinazofanya biashara ya pembejeo na zana za kilimo hutoa mikopo kwa wakulima mmoja mmoja au kupitia vikundi," alisema.

Aidha, alisema mfumo mwingine ni kupitia taasisi za serikali kama Mfuko wa Taifa wa Pembejeo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambazo hutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wakulima ukilinganisha na kampuni binafsi.

"Pamoja na kuwepo kwa mifumo hiyo, baadhi ya wakulima hushindwa kupata mikopo ya pembejeo kutokana na riba kubwa na masharti mengine yanayotolewa na watoa huduma,"alisema.

Kutokana na kero hizo, serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kuwatambua watoa huduma wote wanaotoa mikopo ya pembejeo za kilimo ikiwemo matrekta ili kujua aina ya huduma na mikopo inayotolewa kwa wakulima.

Alisema hatua hiyo itasaidia kutambua kero zilizopo na kuzipatia ufumbuzi ikiwemo kupunguza riba, kuweka utaratibu unamwezesha mkulima kurejesha mkopo kulingana na mapato ya mkulima kwa msimu wa kilimo.

"Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo zinaendelea kutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wakulima ambapo zinatoa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa mkulima mmoja mmoja, vikundi na vyama vya ushirika kwa riba ya asilimia sita hadi 10 kulingana na aina ya mkopo," alisema.

Alisema katika mwaka 2020/2021 hadi Februari, 2021 Mfuko wa Taifa wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 959.5.

"Kati ya mikopo hiyo, mikopo ya matrekta makubwa 16 yenye thamani ya Sh milioni 729.5 imetolewa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imetoa mikopo ya matrekta makubwa 62 yenye thamani ya Sh bilioni 5.6," alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz