Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania na Uingereza kujadili fursa za kibiashara DSM

Majaliwa Pc Data Tanzania na Uingereza kujadili fursa za kibiashara DSM

Sun, 14 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

KONGAMANO la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza litakalofanyika wiki ijayo, litawezesha kufungua milango zaidi ya nchi kuuza bidhaa zake katika nchi hiyo.

Litafanyika Dar es Salaam na linatarajiwa kufunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuhudhuriwa na Mjumbe Maalumu wa masuala ya biashara wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Lord Walney.

Akizungumzia kongamano hilo litakalofanyika keshokutwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo alisema limeratibiwa na wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Ubalozi wa Uingereza nchini pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Mkumbo alisema mwaka huu, bidhaa za Tanzania zilizouzwa nchini Uingereza zimekuwa za thamani ya Sh bilioni 90 ilhali za Uingereza zilizouzwa nchini zina thamani ya Sh bilioni 450 hivyo kupitia kongamano hilo, fursa zaidi zitaongezeka kwa nchi zote mbili.

Alisema katika mkutano huo, kikubwa watakachokifanya watapiga debe ili Tanzania ipate soko la nyama katika nchi hiyo kwani likipatikana itakuwa rahisi kuuzia nchi zote zilizopo katika Umoja wa Ulaya.

“Pamoja na mambo mengine inatarajiwa kuwa kongamano hili litatoa fursa kwa washiriki kujadiliana kwa kina na kubaini fursa mpya za ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Aidha, kupitia majadiliano hayo, pande hizi mbili zitaweza kupanua zaidi wigo wa ushirikiano katika maeneo ya biashara na uwekezaji hususani katika sekta za nishati, madini, miundombinu, kilimo, uchumi wa buluu na utalii,” alisema.

Alisema kongamano hilo pia litapitia changamoto mbalimbali za kisera zilizokuwa zikiwakabili wawekezaji kutoka Uingereza na zitajadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi.

Mkumbo alisema nchi hizo mbili zina uhusiano wa karibu wa muda mrefu ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku kutokana na mashauriano ya mara kwa mara baina ya serikali za pande zote mbili.

“Kwa mfano kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji (TIC), nchi ya Uingereza ni ya pili kwa uwekezaji hapa nchini ikiwa na miradi takribani 945 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.42 na kutoa ajira takribani 275,384,” alisema.

Balozi wa Uingereza nchini, David Concar alisema kuwa Walney atawasili kesho kwa ajili ya kuhudhuria kongamano hilo hadi Novemba 19 mwaka huu na kwa kushirikiana na Waziri Mkuu, Majaliwa watafungua kongamano hilo.

Alisema zaidi ya wafanyabiashara 125 watafuatilia kongamano hilo kupitia mtandao. Wawakilishi kutoka kampuni 20 za nchini humo watahudhuria kongamano hilo linalofanyika Dar es Salaam.

Concar alisema anaamini kuwa mazungumzo hayo yataimarisha jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kuimarisha biashara katika nchi hizo mbili, kuwezesha ukuaji wa sekta binafsi kwa ajili ya kusaidia kutengeneza ajira na kukuza uchumi.

Chanzo: Habarileo