Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania na China wakubaliana mambo makubwa kuhusu Kilimo

1946 CH0 TZW

Thu, 25 Jan 2018 Chanzo: bongo5.com

Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba amekutana na Naibu Waziri wa Kilimo China, Dkt. Qu Dongyu na kukubaliana kushirikiana kuwasaidia wakulima wa Tanzania kulima mazao kwa kuzingatia ubora unaohitajika kwa ajili ya soko la bidhaa za kilimo nchini China.



Dkt. Tizeba ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam ya kumalizika kwa kikao baina ya Mawaziri kujadili njia bora ya kuwasaidia wakulima kuwa na soko la uhakika nchini China.

“Tumekubaliana kuunda kikosi kazi cha wataalam wa nchi hizi mbili kuangalia kwa undani jinsi ya kuboresha kilimo chetu hasa katika suala la masoko kwani wakulima wetu wanazalisha bila kuwa na soko hivyo mkakati uliopo ni wa kuwaleta wawekezaji kutoka China kuingia mkataba na wakulima wa Tanzania na kuwaelekeza vigezo vya uzalishaji wanaoutaka ili wakizalisha wawe na uhakika na soko.”amesema Dkt. Tizeba.

Ameongeza kuwa katika kikao hicho imekubalika kuwa wawekezaji wa China waeleze kwa uwazi na kujaili vigezo vya baadhi ya mazao ili Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Marry Mwanjelwa atakapokwenda China mwezi Mei mwaka huu, akutane na wawekezaji mbalimbali watakaokuja kuwekeza nchini wakiwa na uhakika wa kuzalisha kwa ubora wanaouhitaji ikiwa ni moja ya ushirikiano wa kitaalam kati ya nchi hizo.

Vile vile Dkt. Tizeba amesema kuwa ni lazima kupata fursa ya kutangaza mazao ya Tanzania nchini China hivyo katika majadiliano hayo Serikali ya China imekubali kutoa nafasi ya kuwa na maonesho ya kudumu ya bidhaa za Tanzania nchini mwao.

Akiongelea kuhusu usindikaji wa mazao, Dkt Tizeba amesema kuwa uzalishaji wa mazao ni mkubwa lakini mengi yanaharibika kwa kutokuwa na viwanda vya kusindika kwa hiyo uhifadhi wa mazao kuanzia shambani hadi sokoni unatakiwa uwe wa uhakika hivyo tunawakaribisha watu wa China kuja kuwekeza katika viwanda vya usindikaji wa mazao.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo China, Dkt. Qu Dongyu amesema kuwa nchi hizo mbili zina urafiki wa muda mrefu hivyo Serikali ya China imejidhatiti kusaidiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo yakiwemo ya uwekezaji, teknolojia, kujengea uwezo wananchi pamoja na ukuzaji wa soko.

“Soko la China ni kubwa na Tanzania ina vitu vingi vya kupeleka katika soko letu hivyo tunahitaji wakulima wengi kuleta mazao nchini kwetu, kwa kuzingatia hilo tutahakikisha wakulima wa Tanzania wanaweka juhudi na maarifa katika kilimo pamoja na kushirikiana na wawekezaji wetu ili kufahamu vigezo vya mazao tunayoyahitaji kabla ya kulima,” amesema Dkt. Qu Dongyu.

Kikao hicho ni muendelezo wa mazungumzo yaliyojadiliwa na Marais wa Tanzania na China katika kuboresha kilimo hivyo kikao cha leo kimefanyika kwa ajili ya kuweka mipango ya utekelezaji wa makubaliano na maelekezo ya Marais hao.

Chanzo: bongo5.com