Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa 13 wa Shirikisho la Korosho Afrika (ACA) unaotarajiwa kufanyika Novemba 7 hadi 9, 2019 jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo utawakutanisha wadau wa korosho zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika kujadili ushirikiano baina yao na changamoto zinazowakabili ikiwamo masoko ya zao hilo.
Ni mara ya pili kwa mkutano huo kufanyika Tanzania, mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2008.
Akizungumzia leo Jumanne Julai 16, 2019 mkurugenzi mkuu wa ACA, Ernest Mintah amesema mkutano huo wa siku tatu utawakutanisha wakulima, wafanyabiashara, wabanguaji, wasafirishaji, viongozi wa Serikali na watengenezaji wa vifaa ili kujadili mwelekeo, fursa na changamoto za sekta hiyo.
“Mwaka 2017 korosho ziliizidi tumbaku kwa kuwa zao linalosafirishwa nje kwa wingi likiingiza mapato zaidi,” amesema.
Mwakilishi wa Wizara ya Kilimo, Dk Steven Ngailo amesema changamoto inayozikabili nchi za Afrika ni ubanguaji wa korosho.
Pia Soma
- Bongo movie, Swahilflix kumleta Will Smith Tanzania
- Rais Magufuli asisitiza bei elekezi zao la pamba ni Sh1,200
- NEC kuanza uboreshaji wa Daftari, Kihamia atoa mwongozo
- TCU yavifungulia vyuo vilivyofungiwa kudahili
“Kwa sababu mkutano huu utafanyika msimu wa korosho, hiyo itakuwa ni fursa ya pekee kwa wadau kutoka nje ya nchi kuangalia fursa za uwekezaji kwenye korosho,” amesema Dk Ngailo.