Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania mwenyeji mkutano mkuu shirikisho la korosho Afrika

83326 Korosho+pic Tanzania mwenyeji mkutano mkuu shirikisho la korosho Afrika

Sun, 10 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kwa siku tatu mfululizo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa 13 wa Shirikisho la Wadau wa Korosho Afrika (ACA).

Mkutano huo unafanyika jijini Dar es Salaam sambamba na maonyesho ya bidhaa na teknolojia za kuzalisha na kusindika zao hilo, umewakutanisha wadau tofauti waliopo kwenye mnyororo wa thamani.

Akifungua mkutano huo  rais wa ACA, Florentino Nangue amesema ajenda kuu ya mkutano huo ni kujadili kwa kina mabadiliko yanayojitokeza kwenye soko la korosho duniani.

“Tutajadili mabadiliko ya sera yanayoendelea kwenye sekta hii pia Tanzania ikiwa mfano na jinsi sekta binafsi pamoja na Serikali zinavyoweza kunufaika bila kumuumiza mkulima,” amesema Nangue.

Kutokana na uzoefu tofauti alionao kila mshiriki wa mkutano na maonyesho hayo yanayofanyika katika Hotel ya Serena jijini hapa, amesema anaamini majibu ya changamoto mbalimbali zilizopo yatapatikana.

Mapendekezo yatakayopatikana katika mkutano huo, Nangue amesema yanapaswa kumnufaisha mtu mmoja mmoja kwanza, kuanzia mkulima wa korosho, taasisi zinazojihusisha na zao hilo mpaka Serikali inayotunga sera na kuweka mazingira rafiki kwa biashara ya korosho.

Akiwakaribisha wageni kutoka mataifa mbalimbali yanayolima au kutumia korosho na bidhaa zake, makamu mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula amewapa changamoto washiriki wa mkutano huo kujiuliza na kupata majibu kwa nini Afrika bado inasafirisha korosho ghafi.

Amesema hii ni fursa adhimu kwa Tanzania kuwakutanisha watafiti, taasisi za fedha, watunga sera, wawakilishi wa Serikali na wadau wote wa korosho kubadilishana uzoefu wa kuendeleza zao hili muhimu kwa uchumi wa mataifa yanayolilima pamoja na wananchi wanaoshiriki.

Serikali ya Tanzania, amesema inahamasisha uchumi wa viwanda utakaoiwezesha kuwa na kipato cha kati na inachukua hatua za makusudi kuondoa vikwazo vya kufanya biashara.

Tanzania inazalisha korosho bora zaidi duniani ikiwa ya nne Afrika ikitumia wastani wa hekta 300,000 sawa na asilimia mbili ya eneo zima ililonalo lakini, amesema kiasi kikubwa kinasafirishwa nje ya nje na kwenda kutoa ajira huko.

“Tutumie fursa hii kujadili namna tunavyoweza kuondokana na hali hii,” amesema Angelina.

Ili manufaa ya Tanzania inayochangia asilimia sita ya korosho zote zinazozalishwa duniani yaonekane kwa wananchi hasa wakulima wa kijijini, amesema Afrika na Tanzania kimahsusi inahitaji kuwekeza zaidi kwenye sayansi na teknolojia ili kuzitumia fursa zilizopo kwenye eneo hilo kwa ufasaha.

Amesema takwimu zinaonyesha Afrika inazo zaidi ya hekta 600,000 za ardhi safi inayofaa kwa kilimo lakini hazitumiki hivyo ni uwekezaji pekee utakaowashawishi vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwenye kilimo na kuzitumia hekta hizo kwa manufaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz