Tanzania imepitishwa kuwa Mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Nchi 25 wazalishaji wa zao la Kahawa Afrika(G-25).
Hayo yamesemwa katika Mkutano wa pili wa nchi wazalishaji wa zao la Kahawa Afrika uliofanyika Jijini Kampala,Uganda na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni.
Katika Azimio la Kampala (Kampala Declaration) imetamka bayana kwamba Mkutano wa tatu wa nchi wazalishaji wa Kahawa Afrika utafanyika Tanzania mwaka 2024 na hivyo azimio hilo kuitangaza Tanzania kama Mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa Kahawa Afrika.
Akizungumza katika Mkutano huo,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ameeleza bayana mikakati ya kukuza zao la kahawa nchini.
Amesema Tanzania imeongeza bajeti ya Wizara ya kilimo ambapo juhudi nyingi zimeelekezwa katika utafiti na uzalishaji wa miche bora ambayo husambazwa kwa wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa ambapo uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kutoka Tani 66,543 mwaka 2021/22 hadi kufikia Tani 82,491 kwa mwaka 2022/2023.
Aidha Dkt. Mpango alitumia fursa hiyo kuwaalika nchi wazalishaji wa zao la kahawa katika mkutano wa tatu wa nchi 25 (3rd G-25 Africa Coffee Summit 2024) wazalishaji wa Kahawa Afrika utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2024.