Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania mbioni kuuza parachichi nchini Marekani

Tanzania Mbioni Kuuza Parachichi Nchini Marekani Tanzania mbioni kuuza parachichi nchini Marekani

Fri, 4 Nov 2022 Chanzo: Eatv

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema kufuatia mahusiano mazuri ya kibiashara baina ya Tanzania na Marekani, Tanzania ipo mbioni kunufaika na soko kubwa la Parachichi nchini Marekani baada ya kukamilika kwa taratibu chache za masuala ya usafi wa mazao

Hayo yamesemwa  leo tarehe 03 Novemba, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde na Ujumbe kutoka nchini Marekani ukiongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Jewel Bronaugh

"Serikali inaendelea na  mazungumzo na Marekani, ili tuweze kufikia vigezo vya kibiashara kuuza parachichi yetu nchini mwao.

Tayari taratibu za awali za kuhakikisha tunakidhi vigezo vya kimataifa vya usalama na usafi wa mazao umeanza, kukamilika kwa taratibu hizo kutafungua mlango wa nchi ya Tanzania kuanza kusafirisha kwa wingi parachichi nchini Marekani na hivyo kutengeneza soko la uhakika la zao la parachichi kwa wakulima wa Tanzania.

"Ninaishukuru Serikali ya Marekani kwa kukubali kuirudisha Tanzania kuwa moja ya Nchi zinazotekeleza Programu ya  Feed the Future ambao pia ndani yake upo mradi wenye thamani ya Dola za kimarekani 40m wa kukuza tasnia ya mbogamboga na matunda ambao pia utalenga katika kuongeza mnyororo wa thamani ya zao la parachichi na mazao mengine."

"Ni vyema  programu mbalimbali zinazoletwa kutekelezwa nchini ziwe zinaendana na mipango ya Serikali ambayo inalenga kwenda kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na Watanzania kwa ujumla ili kupunguza fedha nyingi kutumika katika semina na warsha mbalimbali ambazo mwisho wa siku zina mchango mdogo katika kukuza sekta ya Kilimo” Alisema Mavunde

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Kilimo wa Marekani, Dkt. Jewel Bronaugh ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa  dhamira na utashi mkubwa wa kukuza sekta ya kilimo ambayo inathibitishwa na ongezeko la bajeti ya nchi katika kilimo na kuja na mikakati kabambe ya kukuza sekta ya Kilimo nchini.

Naibu Waziri Dr. Bronaugh ameahidi nchi yake kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kuendelea  kutekeleza programu na mikakati mbalimbali yenye lengo la kuendeleza sekta ya kilimo na kuimarisha mahusiano ya kibiashara baina ya Marekani na Tanzania.

 

Chanzo: Eatv