Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kufikia mwaka 2025 Tanzania itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 5,000 za umeme kulingana na miradi inayotekelezwa.
Makamba ameyasema hayo leo, Februari 14, 2023 wakati akuhutubia kwenye hafla ya utiaji saini wa mikataba ya uimarishaji wa gridi ya taifa, Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Kufikia mwaka 2025 uzalishaji wa umeme utakuwa mara tatu zaidi ya umeme uliopo sasa kwani utafikia megawati 5,000 na utakuwa (Rais) umejenga msingi mzuri wa uzalishaji umeme,” amesema Makamba.
Amesema hatua hiyo inatokana na juhudi za dhati zinazofanywa na Serikali kuhakikisha inamaliza tatizo ya umeme nchini.
“Uliponiteuwa kuwa Waziri wa wizara hii (Nishati), nilianza na matatizo kulikuwa na kukatikatika kwa umeme ikaja Waziri mpya kaja na balaa ameingia umeme unakatikakatika, tulichokifanya ni kujifungia na wenzetu wa Tanesco kufanya uchunguzi wa tatizo hasa ni nini.
“Je, ni kweli limeanza katika kipindi ambacho wewe umekuwa Rais na umeniteuwa mimi kuwa Waziri, tukasoma nyaraka mbalimbali ikiwemo ya CAG,” amesema.
Amesema katika uchunguzi huo, walikutana na taarifa hiyo ya CAG ambayo pia iliripotiwa na gazeti la Mwananchi la Aprili 21 2019 lililoandika kichwa cha habari ‘CAG ataja sababu za kukatika katika kwa umeme’.
“Tukachukua taarifa hii, maelekezo yako Rais, malalamiko ya wananchi kama vitendea kazi katika shughuli yetu na katika hilo tukasema tuna machaguo mawili, kutengeneza mitambo na miundombinu ili kumaliza tatizo kwa kudumu na kuziba eneo la awali au kiufanya matengenezo upya,” amesema Makamba.
Kwa mujibu wa Makamba uamuzi uliofanyika ni kutumia mbinu ya pili ambayo ni kuanza matengenezo na uimarishaji gridi ambayo hata hivyo ina maumivu yake.
“Katika kulitekeleza hili kuna maumivu kiasi, lazima kuna muda tutalazimika kuzima mitambo ili tutengeneze hapa ndipo kwenye tatizo,” amesema.
Amesema kwa sasa Tanzania ina njia kuu za kuzalisha umeme wa kilometa 6,000 na mahitaji ni kilometa 12,000.
“Tunaposema tunazalisha umeme wa megawati 1,700 unatosha ni kwamba hautoshi, ni kwamba hauwafikii wahitaji ukiwafikia hautoshi ni mdogo mno,” amesema.