Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kuwekeza tafiti za madini

Mavunde Atoa Mwelekeo Mpya Sekta Ya Madini Tanzania kuwekeza tafiti za madini

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Doto Biteko amezindua Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji na Madini la Mwaka 2023 huku akiahidi Serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kufanya tafiti zitakazosaidia kuwa na akiba maeneo ya uwekezaji wa madini mkakati na muhimu.

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, marekebisho ya mwaka 2022 imetoa mamlaka kwa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kuanza kufanya tafiti mbalimbali zinazohusisha taarifa za miamba ya madini ya kimkakati, nishati, viwandani na madini ya vito.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo leo Oktoba 25, 2023 jijini Dar es Salaam, Biteko amesema pamoja na mahitaji makubwa ya madini mkakati katika soko la dunia, Tanzania bado inakabiriwa na changamoto ya taarifa za kijiolojia.

“Hatua ya kuwekeza kwenye utafiti itasaidia kuongeza maeneo ya uwekezaji mpya chini hivyo kuongeza ajira, kuongeza fedha za kigeni na kukuza mchango wa sekta katika uchumi,” amesema Biteko aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Kongamano hilo limekutanisha kampuni za kimataifa za utafiti na uchimbaji, wafanyabiashara wa madini, wachimbaji wadogo, watunga sera na taasisi za kifedha.

Mkurugenzi wa Kanzidata wa GST, Hafsa Seif amesema tayari walishawasilisha maombi ya bajeti Hazina Kuu ya Serikali kwa ajili ya kuanza tafiti.

“Tunasubiri hazina, kwa sasa sina takwimu ni kiasi gani cha bajeti tuliomba,” amesema. Hafsa akisema taarifa zilizopo kwa sasa zinaonyesha uwezekano wa kupata madini mengi ya kimkakati nchini.

Kisheria, GST hufanya tafiti kubwa za aina tatu ikiwamo ya jiolojia inayofanyika kuangalia aina ya miamba na madini yaliyopo katika miamba bila kujua kiwango halisi, ambayo imefanyika kwa asilimia 97 ya ardhi yote Tanzania.

Utafiti wa pili ni ule jiokemia unaochambua kwa kina aina ya miamba iliyobainika kupitia tafiti za kijiolojia, ambayo imefanyika kwa asilimia 23 nchi nzima.

Utafiti wa tatu wa Jiofizikia unahusisha makundi mawili wa tafiti picha za anga na utafiti wa ardhini. Utafiti wa ardhini unahusisha njia mbili; ukusanyaji wa data za usumaku na zile za umeme.

Utafiti wa anga unaokusanya data kwa njia ya usafiri wa anga unahusisha picha za ukusanyaji wa taarifa za awali na zile za kina ambazo zimefanyika kwa asilimia 16 tu nchi nzima.

Tafiti hizo zinafanyika katika vitalu 322 vilivyogawanywa katika ardhi ya Tanzania. Kila kitalu kina ukubwa wa kilometa za mraba 2,916.

Awali, kabla ya Biteko, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Dira ya 2030 inakusudia kuongeza akiba ya maeneo yenye viashiria vya madini kutoka asilimia hiyo 16 hadi asilimia 50 kwa miaka sita.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, eneo hilo la asilimia 16 limewezesha sekta hiyo kufikia mchango wa asilimia 9.1 ya Pato la Taifa (GDP), asilimia 15 ya mapato ya ndani, Dola 3.3 bilioni ya mauzo ya nje, mchango wa asilimia 56 ya fedha za kigeni na Dola milioni 50 kwa huduma na manunuzi ya ndani mwaka 2022/23.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live