Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kuuza nyama Saudi Arabia

1b4bfe496af6518e69af8f6c12e0f1f6.jpeg Tanzania kuuza nyama Saudi Arabia

Mon, 9 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema ziara ya ujumbe kutoka Saudi Arabia ni sehemu utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kupata masoko nje.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Elisante Ole Gabriel, alisema Rais Samia aliielekeza wizara hiyo itafute masoko hayo hivyo inaendelea kuyatafuta.

“Haya masoko ya nje ya nchi ni mazuri kwa sababu yanatupatia fedha za kigeni, lakini pia yanawahakikishia wafugaji wetu soko la uhakika kwa mazao ya mifugo yao,” alisema.

Alisema hayo wakati akizungumzia ziara ya ujumbe huo Dar es Salaam ulioongozwa na Mkaguzi wa Mamlaka ya Dawa na Chakula, Saudi Arabia, Ahmed Alhajouj.

Ole Gabriel alisema kabla ya kukutana nao, ujumbe huo ulikagua maeneo yanayohusika na uchakataji wa mazao ya mifugo yakiwemo machinjio, maabara na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Alitoa rai kwa wafugaji kuboresha ufugaji uwe wa kisasa zaidi ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.

“Ni rahisi kwa serikali kutafuta masoko lakini je, mifugo iliyopo inakidhi soko hilo? Hivyo niwaombe wafugaji na wafanyabiashara watumie fursa hii vizuri kuboresha uchumi wao na wa taifa pia,” alisema.

Alisema kwa sasa sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.4 katika pato la taifa na kwamba, lengo la wizara ni kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025.

Msajili wa Bodi ya Nyama, Dk Daniel Mushi, aliishukuru serikali kwa jitihada inazozifanya kwa kushirikiana na wadau kufungua masoko nje ya nchi ili kuuza nyama.

Mushi alisema ujumbe huo umewapa changamoto kwa kuwa ili waweze kufikia masoko hayo, ni lazima kuboresha lishe ya mifugo ili wanyama wakue haraka na wawe na nyama nyingi yenye ubora.

Hivi karibuni Rais Samia alikutana na mtoto wa Mfalme wa Saudi Arabia na kuielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi itafute masoko nje ya nchi ikiwemo nchi ya Saudi

Chanzo: www.habarileo.co.tz