Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kutumia Balozi kutafuta soko la kahawa duniani

Sokoooo Tanzania kutumia Balozi kutafuta soko la kahawa duniani

Tue, 11 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Bunge la Tanzania limeelezwa Serikali imefanya mazungumzo na balozi za Tanzania nchi za nje ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kutafuta soko na kuongeza bei ya kahawa inayozalishwa nchini.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ameyasema hayo leo Jumanne Juni 11, 2024 wakati wa kujibu swali la nyongeza la mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Profesa Patrick Ndakidemi.

Mbunge huyo ametaka kujua mikakati ya Serikali ya kutafuta wanunuzi na masoko yenye tija kwa wakulima wa Tanzania.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema moja ya mkakati ni kuondoa uuzaji wa zamani wa kahawa na kuhamia katika kuuza wa mnada kwa njia ya kidigitali kupitia Mfumo wa Soko la Bidhaa (TMX).

Amesema katika mfumo huo wanunuzi wanakutana kutoa bei zao na yule anayetoa bei ya juu ndiye anayekubaliwa kununua kahawa.

“Mkakati wetu wa pili tumeshazungumza na balozi zote nchini ambao wamekuwa na jitihada kubwa za kutafuta soko la kahawa yetu kule nje ya nchi, hiyo naamini itasaidia kuongeza soko la kahawa,” amesema.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha 45 cha mkutano wa Bunge la bajeti jijini Dodoma leo, Juni 11, 2024. Picha na Hamis Mniha

Amesema pia wamezungumza na balozi za Tanzania nchi za nje kutafuta soko la kahawa hatua ambayo itasaidia kuongeza bei ya zao hilo hapa nchini.

“Niwaambie wakulima wa kahawa kuwa mambo mazuri yanakuja hivyo endeleeni kulima zao hilo,”amesema.

Naye mbunge wa viti maalumu, Anatropia Theonest ametaka kujua mkakati wa Serikali wakivisaidia vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) baada ya kuuza kahawa ghafi wakauza kahawa iliyochakatwa (fine coffee) kwa faida.

Pia, ametaka kujua kauli ya Serikali kuhusu kampuni zinazonunua kahawa AMCOS kwa bei ya chini badala ya bei sawa na mnada.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema moja ya mkakati wa Serikali ni kuzijengea uwezo AMCOS kwa kuwavutia wawekezaji wa kuanzisha viwanda hatua ambayo itafanya kawaha kuongezwa thamani.

Amesema pia Serikali imetangaza mnada wa kahawa kwa njia ya kidigitali unaofanyika kwa mfumo wa TMX na kuzitaka AMCOS kutumia minada hiyo.

“Kwa sasa haturuhusu mtu kwenda kununua moja kwa moja kwa mkulima ambako wanaonyonya na huo ndio msimamo wa Serikali,”amesema.

Katika swali la nyongeza, Anatropia ametaka kujua ni kampuni gani zimeshiriki ununuzi wa kahawa mkoani Kagera kwa mwaka 2023.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema katika msimu wa masoko ya kahawa wa 2023/2024 jumla ya kampuni 23 na vyama vya ushirika vitatu vilishiriki kwenye ununuzi wa kahawa ya maganda na kahawa maalum katika Mkoa wa Kagera.

Silinde amesema kampuni zilizoshiriki ununuzi wa kahawa maalumu ni Kaderes Peasants Development Plc, Karagwe Estate Ltd, KCU ltd, pamoja na vyama vya ushirika vya Juhudi AMCOS, Nkwenda AMCOS na Mkombozi AMCOS.

Katika swali la nyongeza, mbunge wa viti maalumu, Neema Lugangira ametaka kujua mkakati wa Serikali wa utaratibu wa kuuza vanila hususani Mkoa wa Kagera.

Akijibu swali hilo, Silinde amesema zao la vanila limeingizwa katika mnada wa mfumo wa TMX na kuwa ndio mfumo utakaotumiwa sasa kuuza katika maeneo yote yanayolima vanila.

Chanzo: Mwananchi