Wakati nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zikijipanga kutumia fursa ya Kongamano la 10 la Mafuta na Gesi Afrika Mashariki mwaka 2023 (EAPCE’23), Tanzania inajiandaa kusambaza gesi kwa nchi wanachama wa EAC.
Kongamano hilo litakalofanyika Mei 9 hadi 11 mwaka huu mjini Kampala litahusisha mataifa yote saba ya EAC ambapo yatatumia jukwaa hilo kueleza mikakati ya kuvuna na kutumia nishati ya mafuta na gesi kupata maendeleo endelevu.
Waziri wa Nishati, January Makamba wakati akifungua kikao cha kuwashawishi wadau wa sekta ya mafuta na gesi nchini kushiriki katika kongamano hilo, alisema Tanzania kwa sasa inajiandaa kuanza mradi wa kupeleka gesi katika baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki.
January aliyataja mataifa hayo yaliyoonesha nia ya kuhitaji gesi hiyo kuwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda na Zambia na kuongeza kuwa serikali inaweka mikakati ya namna ya kufikisha nishati hiyo katika nchi hizo kama sehemu ya kuuza gesi hiyo nje ya nchi.
Alisema kongamano hilo litakalohudhuriwa na wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 3,000, ni jukwaa muhimu kuuza sekta ya mafuta na gesi katika soko la EAC lenye watu zaidi ya milioni 300.
Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato alisema kongamano hilo ni fursa kwa nchi za Afrika Mashariki kueleza hatua kwa hatua mahali zilipofikia kuhusu suala zima la mafuta na gesi kuanzia uchimbaji, uvunaji mpaka matumizi ya mafuta na gesi katika nchi zao.