Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kupunguza uzalishaji gesijoto kwa 30%

Df18bb68f82a9ec95fa5d45ebaee42f7.jpeg Tanzania kupunguza uzalishaji gesijoto kwa 30%

Sun, 15 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo amesema Tanzania imepanga kupunguza uzalishaji wa gesijoto kwa asilimia 30 hadi 35 ifi kapo mwaka 2030.

Pia ameyaomba mashirika ya kimataifa kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusaidia misaada ya kifedha ili kufanikisha jitihada hizo.

Dk Jafo alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa mawaziri wa nchi zinazotekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kupitia Local Climate Adaptive Living Facility –uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.

Alisema Tanzania inaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kikubwa kama ilivyo katika mataifa mengi duniani ikiwemo kuongezeka kwa joto katika baadhi ya maeneo, ukame, kuvurugika kwa misimu ya mvua na mafuriko na kusababisha hasara kubwa za kijamii na kiuchumi katika sekta za kilimo, ufugaji, nishati, uvuvi na miundombinu.

Alitolea mfano katika kipindi cha muongo mmoja uliopita Tanzania ilipata hasara ya kiasi cha dola za Marekani milioni 96.6 katika sekta ya kilimo pekee kutokana na ukame. Aidha, Jafo alieleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaigharimu nchi kwa asilimia moja hadi tatu ya Pato la Taifa ambapo kwa mujibu wa Benki ya Dunia hatua zisipochukuliwa mabadiliko ya tabianchi yatachangia ongezeko la umaskini kwa asilimia mbili hadi tatu ifikapo mwaka 2030. Kwa upande wa Zanzibar, Dk Jafo alisema takribani asilimia 30 ya ardhi ipo chini ya wastani wa mita tano juu ya usawa wa bahari na kwamba mabadiliko ya tabianchi yamesababisha baadhi ya visiwa kupotea kutokana na ongezeko la kina cha bahari, visima kuingiwa na maji ya chumvi na kuharibiwa kwa ardhi ya kilimo kutokana na maji ya chumvi kuvamia baadhi ya maeneo. Alibainisha kuwa Tanzania imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuimarisha mifumo ya kitaasisi na kisera pamoja na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live