Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kunufaika kwa mambo manne mkataba mpya na Airtel

36954 Pic+airtel Tanzania kunufaika kwa mambo manne mkataba mpya na Airtel

Thu, 17 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mazungumzo ya miezi minane kati ya Serikali na kampuni ya Bharti Airtel ya India yamehitimishwa jana kwa utiaji saini wa makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine, yatainufaisha Tanzania katika maeneo makubwa manne.

Katika makubaliano hayo yaliyotiwa saini Ikulu ya Dar es Salaam jana na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi na Mwenyekiti wa Bharti Airtel, Sunil Mittal na kushuhidiwa na Rais John Magufuli na viongozi wengine wa Serikali na Airtel, kampuni hiyo ya simu imekubali kupunguza umiliki wa hisa zake za kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kutoka asilimia 60 hadi 51, hivyo kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yoyote kutoka serikalini.

Mbali ya kuongeza hisa hizo, Serikali sasa itapata gawio la kila mwaka kutokana na umiliki wake wa asilimia 49 na inakadiriwa kwamba itakuwa ikipata Sh10 bilioni.

Pia, Bharti Airtel itatoa Sh1 bilioni kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Aprili ili kuonyesha nia njema na Sh2.3 bilioni kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii.

Maeneo mengine ya makubaliano ambayo yalibainishwa na Profesa Kabudi ni bodi ya wakurugenzi ya Airtel Tanzania itakayoundwa na wajumbe saba; Serikali ikiwakilishwa na wajumbe tatu na wanne wa Bharti Airtel; mwenyekiti atateuliwa na Serikali na kuhusu nafasi tatu za juu za menejimenti ambazo moja, ya ofisa mkuu ufundi itashikwa na Mtanzania atakayeteuliwa na Serikali.

Alisema pande zote mbili zitashirikiana kuandaa upya nyaraka muhimu za kusaidia uendeshaji wa kampuni, zitashirikiana kuongeza tija na ufanisi wa Airtel Tanzania na kushirikiana kutumia miundombinu ya Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ikiwa kuna hoja za kibiashara.

Akizungumza baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Rais Magufuli aliipongeza timu iliyoiwakilisha Serikali ikiongozwa na Profesa Kabudi na ile ya Airtel kwa kufikia makubaliano hayo na kueleza matumaini yake kwamba sasa Airtel Tanzania itaanza kutoa gawio na masilahi mengine yanayostahili kwa Tanzania, mambo ambayo hayakufanyika kwa zaidi ya miaka minane ya uhai wa kampuni hiyo nchini.

Akizungumzia fedha zilizotolewa na Mittal kwa Serikali, Rais Magufuli aliagiza ziunganishwe na Sh1 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za Siku ya Uhuru mwaka jana kwa ajili ya kujenga hospitali jijini Dodoma.

“Huu ndio uwekezaji ninaoutaka, uwekezaji ambao tuna faida nao. Airtel ilikuwapo tangu miaka minane, tisa iliyopita lakini tulikuwa hatupati kitu. Sasa tutapata fedha na hili liwe somo kwetu Watanzania wote kuwa Serikali inapotetea masilahi ya Watanzania haizungumzi kutoka hewani, tujifunze kuwaheshimu watalaamu wetu” alisema Rais Magufuli.

Alisema Tanzania ni nchi nzuri ya kuwekeza na kuahidi kwamba itadumisha utamaduni wa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kutambua kuwa njia hiyo itasaidia kuzalisha ajira na kuiwezesha Serikali kupata mapato.



Chanzo: mwananchi.co.tz