Tanzania imechaguliwa kuwa moja ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.
Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) pembezoni mwa Mkutano wa Nne wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia unaendelea Roma, Italia.
Mhandisi Cestari alieleza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaanza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Italia, ambapo Serikali ya nchi hiyo itafadhili miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika. Hatua hiyo itahusisha pia kugharamia gharama za upembuzi yakinifu ya miradi itakayopendekezwa.
Kama hatua ya utekelezaji ya mpango huo, ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia ikiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe. Dkt. Edmondo Cirielli unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano huo wa pande mbili utakaohusisha utekelezaji wa miradi itakayopitishwa na pande mbili.
“Serikali ya Italia imetenga kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo katika nchi nane za kipaumbele za Afrika ikiwemo Tanzania,” alisema Mhandisi Cestari.
Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuonesha nia ya kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ambapo sekta ya nishati, elimu na kilimo zimepewa kipaumbele.