Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kufuata nyayo za Indonesia matumizi nishati safi ya kupikia

Gesi Urahis Serikali Tanzania kufuata nyayo za Indonesia matumizi nishati safi ya kupikia

Thu, 25 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika kuhakikisha Tanzania inafanikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, Serikali itatumia uzoefu kutoka Taifa la Indonesia.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, Indonesia ni miongoni mwa mataifa yaliyofanikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mwaka jana, Rais Samia alizindua mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania, akilenga kile alichoeleza kupunguza athari za matumizi ya nishati isiyofaa.

Rais Samia amesema hayo leo, Alhamisi Januari 25, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Bogor, nchini Indonesia alikokwenda kwa ziara ya siku tatu.

Baada ya mazungumzo ya ndani na Rais wa Indonesia, Joko Widodo, Rais Samia amewaambia waandishi wa habari kuwa Serikali yake itatumia uzoefu wa Indonesia kufanikiwa kwenye mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

"Kwa sababu Indonesia imefanikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, nitashirikiana nayo kuhakikisha Tanzania inapata ujuzi na uzoefu," amesema.

Sambamba na hilo, Rais Samia ameikaribisha Indonesia kuwekeza katika sekta ya nishati jadidifu nchini Tanzania, akisema ni eneo lenye fursa nyingi.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi, amesema mataifa hayo yamesaini mikataba ya makubaliano ya ushirikiano katika maeneo manne.

Ameyataja maeneo hayo ni ushirikiano katika sekta ya madini, uchumi wa buluu na uvuvi, kilimo na diplomasia kwa ujumla.

Katika mazungumzo yao, amesema wamejadili kuhusu hatua ya utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais Widodo nchini Tanzania Agosti, 2023.

"Msisitizo wetu ulikuwa ni kuhakikisha utekelezwaji thabiti wa kile tulichokubaliana wakati ule," amesema.

Katika ziara hiyo, nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC), msamaha wa visa kwa wamiliki wa hati za kusafiria za kidiplomasia, huduma za afya, nishati, mafuta na gesi na madini.

Kwa mujibu wa Rais Samia, mengine waliyozungumza katika kikao cha ndani ni kuridhishwa kwao na maeneo ya ushirikiano waliyonayo na kupanga kuongeza zaidi.

Kuhusu biashara na uwekezaji, amesema mataifa hayo yameona umuhimu wa kuhamasisha ushirikiano kati ya nchi hizo.

"Ndiyo maana leo baadaye nitashiriki jukwaa la uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Indonesia litakalohusisha jumuiya za wafanyabiashara na wadau wengine kutoka mataifa yetu," amesema.

Ameeleza Tanzania itatumia jukwaa hilo kueleza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo.

"Neno langu kwa sekta binafsi, muda mzuri wa kuwekeza nchini Tanzania ilikuwa miaka miwili iliyopita, lakini muda mzuri zaidi ni sasa," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live