Tanzania inatarajiwa kufanya mageuzi ya sekta ya kilimo yatakayowezesha kuongeza vipato vya wakulima, kuimarisha lishe na kupunguza umasikini.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, hilo linatarajiwa kufanyika kupitia mpango wa 'Hand in Hand' unaoratibiwa na kuongozwa na Serikali.
Mweli ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, Septemba 29, 2023 alipofungua mkutano wa majadiliano ya wadau wa kilimo kuhusu fursa za sekta hiyo, ulioandaliwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mweli amesema mpango huo unalenga kuimarisha uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mazao ya alizeti, ngano na soya.
"Ushirikiano huu wa wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo ni muhimu na kipaumbele cha Serikali," amesema.
Amesema kupitia mpango huo, Tanzania inatarajiwa kufanya mageuzi ya kilimo cha mazao ya chakula ili kukomesha umasikini, njaa na lishe duni.
Hata hivyo, mkutano huo umefanyika kuelekea jukwa la uwekezaji linalotarajiwa kufanyika Oktoba 17 hadi 20, mwaka huu nchini Italy.
Kuhusu jukwaa hilo, Mwakilishi Mkazi wa FAO, Dk Nyabenyi Tipo amesema litatoa fursa kwa mataifa kuonyesha fursa za uwekezaji yalizonazo na kuwavutia wawekezaji.
"Titajikita kwenye uwekezaji wa sekta ya kilimo na mnyororo mzima wa thamani kama ilivyoelezwa katika programu ya Hand in Hand," amesema.