Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kuanza kutoza gharama za simu zinazolingana jumuiya ya Afrika Mashariki

Sat, 6 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha.Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Kirunda Kivejinja amesema nchi za Burundi na Tanzania zitajiunga na nchi nyingine za jumuiya hiyo kutoza gharama zinazolingana za simu ifikapo Desemba.

Akijibu swali la Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki(Eala) kutoka Rwanda, Celestine Rwigema aliyetaka kujua iwapo Baraza la Mawaziri la EAC linafahamu gharama za mawasiliano ya simu katika nchi ambazo hazijaoanisha gharama zimekua ni mzigo kwa watumiaji.

Dk Kivejinja amesema nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Sudan Kusini zimekamilisha muundo huo (EAC Roaming Framework) ambao ulipitishwa na Baraza la Mawaziri na baadaye marais  wa nchi za EAC kuagiza utekelezaji wake Julai 31,2015.

 

"Napenda kuwajulisha kuwa ifikapo Desemba mwaka huu nchi za Burundi na Tanzania zitakua zimejiunga kwenye muundo wa pamoja wa mawasiliano ya simu katika nchi zetu hatua itakayopunguza gharama unapopiga simu ndani ya jumuiya yetu,"alisema  Dk Kivejinja.

Amesema kuchelewa kwa Burundi na Tanzania kujiunga na nchi nyingine kumesabishwa na michakato ya ndani ya nchi husika ambayo kwasasa imefanyiwa kazi na inatarajiwa ifikapo Desemba itakua mwisho kulingana na maelekezo yaliyotolewa na marais wa EAC.

 

Hatua hiyo ilimfanya Mbunge kutoka Uganda, Paul Musamali kuhoji kwanini Tanzania na Burundi wanachama wa EAC wa mwanzo hadi sasa hawajaingia kwenye mfumo wa gharama za mawasiliano walizokubaliana wakati mwanachama mpya Sudan Kusini ameweza kujiunga.

Wakati huo huo, Mbunge kutoka Kenya, Abdikadir Omar Aden alitaka kufahamu kwanini Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ambayo ni miongoni mwa taasisi za EAC haijaingizwa kwenye makadirio na mapato ya mwaka fedha 2018/19.

Pia ametaka kufahamu kwanini  hesabu zake hazijakaguliwa na Kamisheni ya Ukaguzi wa Hesabu za EAC kulingana na sheria inavyotaka.

 

Dk Kivejinja amewataja wanahisa wa EADB kuwa ni Kenya yenye asilimia 27.03,Tanzania asilimia 23.77, Uganda asilimia 27.3 na Rwanda asilimia 9.51 na kuzifanya nchi za EAC kuwa na asilimia 87.33.

Amesema wanahisa wengine ni African Development Bank (AfDB) asilimia 8.82, FMO Netherlands asilimia 2.67, DEG Germany yenye asilimia 0.71, Yugoslavia Consortium asilimia 0.2, SBIC African Holdings asilimia 0.17, Commercial Bank of Africa asilimia 0.04, Nordea Bank-Sweden asilimia 0.04, Standard Chartered Bank asilimia 0.01 na Baclays Bank PLC  asilimia 0.01.

 

Amesema kutokana na muundo huo baada ya benki hiyo kuanza upya mwaka 1980 baada ya iliyokua EAC kuvunjika mwaka 1977 hakuna sehemu yeyote panapotajwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwasababu wakati wa kuianzishwa upya EADB jumuiya hiyo haikuwapo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz